May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba ajitosa mauaji Palestina

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF), nchini Tanzania, Prof. Ibrahim Lipumba, ameishauri Serikali ya Tanzania, ifuate nyayo za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, za kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya raia wa Palestina. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Prof. Lipumba ametoa wito huo leo Jumatano, tarehe 19 Mei 2021, siku nane baada ya kuibuka mapigano katika Ukanda wa Gaza, kati ya Jeshi la Israel na wanamgambo wa Palestina, yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 200.

“Tunatoa wito kwa Serikali ya Tanzania, kurejea kwenye msimamo wa Mwalimu Nyerere wa kupinga dhulma na uonevu duniani kote na kuwaunga mkono kwa dhati Wapalestina wapate haki zao,” amesema Prof. Lipumba.

Akizungumzia mzozo huo wa muda mrefu baina ya Palestina na Israel, Prof. Lipumba amekumbushia uamuzi wa Mwalimu Nyerere wa kuitenga Israel kufuatia sera zake zinazodaiwa kuwakandamiza raia wa Palestina.

“Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ina historia ndefu ya kutetea na kupigania haki za Wapalestina,” amesema Prof. Lipumba.

Mwanasiasa huyo amesema “baada ya vita vya Yom Kippur baina ya Waarabu na Israel ya Oktoba 1973, Tanzania ilivunja uhusiano na Israel na kuunga mkono Wapalestina na mataifa ya Kiarabu ambayo ardhi yao iliporwa na Israel.”

Kuhusu mauaji yanayoendelea Gaza, Prof. Lipumba amesema, chama chake kinalaani mauaji hayo

“CUF tumesikitishwa na kukasirishwa na mauaji ya kinyama yanayofanyiwa Wapalestina katika ukanda wa Gaza kwa kupiga mabomu makazi ya wananchi na kusababisha vifo vya Zaidi ya watu 200 wakiwemo zaidi ya watoto 60.”

Israel na Palestina ziko kwenye mgogoro wa muda mrefu, uliosababishwa na kugombania ardhi.

error: Content is protected !!