September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba aipasua CUF

Spread the love

NDANI ya Chama cha Wananchi (CUF) kuna makundi mawili makuu, moja likimtaka Prof. Ibrahim Lipumba aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho na lingine likitaka atoswe, anaandika Happiness Lidwino.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa, kundi linalotaka atoswe limedhamiria kuvunja katiba huku kundi linalotaka arejeshwe kwenye nafasi hiyo limeapa kusimama na katiba ya chama hicho.

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba, kundi linalotaka atoswe linafanya mkakati wa kuvunja Katiba ya mwaka 1992 Toleo 2013 Ibara ya 117 inayoeleza kwamba, “… kama hakuainisha tarehe ya kujiuzulu kwake basi mara baada ya katibu wa mamlaka iliyomteua ama kumchagua kupokea barua hiyo na kumjibu.”

Taarifa zinaeleza kuwa, maombi ya Prof. Lipumba kujiuzulu yalimfikia katibu wa mamlaka ambaye ni Maalim Seif Shariff Hamad na kwamba, kwa mujibu wa ibara hiyo, alipaswa kupeleka maombi hao katika Mkutano Mkuu wa chama hicho kuijadili barua hiyo na baadaye kujibu baada ya Mkutano Mkuu kujadili jambo ambalo mpaka sasa halijafanyika.

Prof. Lipumba aliteuliwa kutwaa nafasi hiyo na Mkutano Mkuu mwaka 1999. Ibara hiyo inaipa mamlaka mkutano huo kukubali ama kukataa kujiuzulu kwake.

“Kwa mujibu wa Katiba ya CUF Prof. Lipumba bado ni mwenyekiti wa CUF. Uenyekiti wake unakoma pale tu katibu wa mamlaka (baada ya Mkutano Mkuu) kuridhia maombi yake ya kujiuzulu na kumjibu kwa barua, Prof. Lipumba mpaka sasa hajajibiwa,” ameeleza mjumbe mmoja wa Mkutano Mkuu aliyeomba kuhifadhiwa jina lake na kuongeza;

“Watu walidhibitiwa sana kwenye mapato ya chama ndio maana wanataka asirudi, hili ndio linalosababisha hata kutaka kuvunja Katiba. Lakini cha kujiuliza kwanini wanataka kukwepa ibara ya 117? Wanajua kwenye Mkutano Mkuu wajumbe hawawezi kukubali.”

Kwa mujibu wa taratibu za CUF, Baraza Kuu halina mamlaka ya kukubali ama kukataa.

“Mpaka sasa katibu wa mamlaka halijaleta taarifa ama maombi ya kujiuzulu kwa Prof. Lipumba, tunaisuburi ije na hakuna chochote kitakachofanyika mpaka utaratibu huu ufuatwe. Hatopatikana mwenyekiti mwingine mpaka taarifa hiyo itufikie,” amesema.

Mvutano wa CUF umedhihiri juzi kwenye kongamano lililoandaliwa na Kata ya Makurumla Manispaa ya Kinondoni ambapo wajumbe waliibua hoja ya ukimya wa taarifa kuhusu maombi ya kujiuzulu ya Prof. Lipumba.

Katika kongamano hilo, Mohamed Mgomvi, mmoja wa wanachama wa CUF alisema, upande wa bara chama hicho kimebaki kwenye uyatima na kwamba hakuna mtu madhubuti anayeweza kukiendesha kama Prof. Lipumba.

“Nashangaa viongozi wetu mnasema habari zisizoeleweka juu ya kujiuzulu kwa Lipumba badala ya kusema ukweli nini kinaendelea huko ndani, tangu alipoondoka Lipumba hakuna maendeleo alafu mnasema tupo pamoja naye, haiingii akilini hata kidogo,” alisema.

Maganga Dachi, mwanachama wa CUF katika mkutano huo pia alisema, kwa mujibu wa Katiba ya CUF, barua ya kujiuzulu inatakiwa ifike katika Mkutano Mkuu uliomchagua jambo ambalo halijafanyika.

“Kwa hatua hiyo chama kinavunja Katiba maana hadi leo hakuna kinachoendelea kama hivyo suala la Lipumba, linatakiwa kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu nasi tunamtaka Lipumba arudi katika nafasi yake ili chama kiendelee na shughuli za kimaendeleo,” alisema Dachi.

Ushawishi ndani ya chama hicho unaendelea kufanywa na baadhi ya wanachama pia viongozi wa chama hicho kumrejesha Prof. Lipumba kwenye nafasi hiyo.

Prof. Lipumba alijiuzulu nafasi yake mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na uamuzi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuridhia Edward Lowassa kuepusha bendera ya umoja huo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 kupitia Chadema.

Akizungumza na MwanaHALISI Online leo Sheweji Mketo, Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mipango wa CUF amesema, kwa mujibu wa Katiba ya CUF, Prof. Lipumba anayo nafasi ya kurejea kwenye nafasi hiyo.

Mketo amesema, Katiba ya chama inamruhusu mwanachama aliyejiuzulu uongozi kurudi kuwania tena nafasi yoyote kwani kujiuzulu ni haki ya mwanachama.

Akijibu hoja ya Prof. Lipumba kurejea kwenye nafasi hiyo amesema, “anaruhusiwa kurudi kama kawaida, atajaza fomu za kuomba kuwania uongozi na atapigiwa kura na baraza la chama kama wagombea wengine.”

Amesema utaratibu wa chama hicho katika kumpata mwenyekiti ni kuitisha Mkutano Mkuu ndani ya miezi sita ili kumchagua mwenyekiti mpya.

“Tatizo ni kwamba, mpaka hadi sasa bado hatujafanya kikao kutokana na kukosa fedha hivyo chama kimeongeza miezi mingine sita ambapo mkutano mkuu unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu,” anasema.

error: Content is protected !!