May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba afukua ya Maalim Seif mwaka 1975

Spread the love

 

PROFESA Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), amemueleza Maalim Seif Sharif Hamad kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilimzuia kubaki lakini aligoma. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kwenye simulizi yake kuhusu maisha ya Maalim Seif aliyefariki Jumatano tarehe 17 Februari 2021, Prof. Lipumba amesema, mwaka huo ndio alianza kumfahamu kiongozi huyo ambaye amefariki akiwa Makamu wa Rais wa Zanzibar.

“Maalim Seif alikuwa mwanafunzi bora mwenye kipaji cha juu. Mwaka 1975 aliongoza katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala kwa kupata Shahada ya Kwanza ya daraja la juu.( B.A. (Hon) First Class).

“Chuo kilijaribu kumshawishi abakie kuwa Mwalimu wa Chuo Kikuu. Hata hivyo, aliitikia wito wa kurudi Zanzibar na kufanya kazi kama Katibu na Msaidizi wa Rais Aboud Jumbe,” anasimulia Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba ameeleza namna alivyojuana na Maalim Seif, akisema kwamba kwa mara ya kwanza walikutana mwaka 1973, wakati wakiwa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Amesema, wakati huo Maalim Seif alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wakati Prof. Lipumba akiwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Idara ya Uchumi.

“Tukiwa Chuo Kikuu, Maalim Seif alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Muslim Students Association of University of Dar es Salaam (MSAUD), mimi nikiwa Mweka Hazina wa Umoja huo.

“Pia tulishirikiana katika shughuli za kiuongozi wa wanafunzi wakati akiwa Kiongozi wa Wanafunzi wa Zanzibar na mimi nikiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa TANU, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” amesema.

Akizungumzia uimara wa Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa CUF kabla ya kuhamia Chama cha ACT-Wazalendo mwaka 2019, amesema kiongozi huyo alikuwa na msimamo usioyumba.

“Kwa hakika Taifa limepoteza mwanasiasa mahiri ambaye itakuwa ni vigumu sana kumsahau katika siasa za nchi hii, hususan kwa Zanzibar.

“Tunamuomba Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake na amuepushe na adhabu zake na amthibitishe kuwa ni mja wa Peponi,” amesema Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba amesema, chama chake kitamtambua mwanasiasa huyo kama mtu aliyetoa mchango mkubwa kukijenga CUF.

“CUF kinamtambua marehemu Maalim Seif kama muasisi na miogoni mwa viongozi wakuu wa chama kiliposajiliwa mwaka 1993,’ amesema Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba amesema, Maalim Seif enzi za uhai, alikiongoza CUF katika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Taifa kuanzia mwaka 1993 – 1999 alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.

Amesema, Maalim Seif alihudumu katika nafasi ya ukatibu mkuu hadi alipohamia katika ACT-Wazalendo Machi 2019.

“Maalim Seif alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa CUF na kushika wadhifa huo mwaka 1993 – 1999. Mwaka 1999 nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Maalim Seif alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu.

Amefanya kazi ya Katibu Mkuu wa CUF mpaka Machi 2019 alipohamia ACT-Wazalendo,” amesema Prof. Lipumba.

Licha ya kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya CUF, Hayati Maalim Seif aliipeperusha bendera ya chama hicho katika chaguzi za urais visiwani Zanzibar, ambapo alikuwa mgombea urais wa CUF katika uchaguzi wa 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015.

Mbali na kuwa mchango mkubwa katika kuijenga CUF, Prof. Lipumba amesema, Maalim Seif alikuwa jabali katika ujenzi wa siasa na jamii Zanzibar na Tanzania Bara.

Prof. Lipumba na Maalim Seif enzi za uhai wake wakiwa kwenye shughuli za kisiasa

“Maalim Seif ametoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kisiasa na kijamii. Alikuwa Waziri wa Elimu wa Zanzibar, Waziri Kiongozi wakati wa mabadiliko ya sera za Uchumi za Zanzibar chini ya Uongozi wa Rais Ali Hassan Mwinyi 1984-85, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar 2010 – 15 na 2020 mpaka alipofariki,” amesema Prof. Lipumba.

Kufuatia mchango wa Maalim Seif katika ujenzi wa CUF, Prof. Lipumba amesema chama hicho kitaombeleza kifo chake kwa muda wa siku saba, kwa kupeperusha bendera zake nusu mlingoti.

“Kufuatia Msiba huu Mkubwa bendera za CUF- Chama Cha Wananchi zitapepea nusu mlingoti kwa muda wa siku saba kuanzia leo Jumatano Februari 17, 2021,” amesema Prof. Lipumba.

error: Content is protected !!