January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba ‘afika bei’

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba akitanganza kung'atuka wadhifa wake wa Uenyekiti wa CUF

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, ametangaza kung’atuka wazifa wake, kwa kile alichoeleza, “kuwa kikwazo” katika harakati za kukindoa madarakani Chama Cha Mapinduzi. Anaandika Saed Kubenea … (endelea).

Amesema, ndani ya CUF haaminiki tena katika mapambano ya sasa ya kutaka kukiondoa chama tawala mamlakani, hivyo “nimeamua kujiweka pembeni” ili kazi hiyo iweze kufanyika kwa ufasaha.

Amesema, “Katika hali halisi iliyopo ndani ya uongozi wa chama chetu, mimi naonekana kikwazo. Naonekana nakwamisha mapambano ya ukombozi. Kwamba siwezi kuwa na mchango wa maana kama mwenyekiti katika mapambano ya kudai haki sawa kwa wote katika kipindi hiki.”

Aidha, Prof. Lipumba amesema, ameamua kujiuzulu kwa kuwa baadhi ya viongozi wenzake ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wamewakaribisha wanachama na viongozi wa CCM waliokuwa mstari wa mbele kupinga Rasimu ya Pili ya Katiba.

Hata hivyo, Prof. Lipumba alikuwa mmoja wa wenyeviti wanne wanaounda UKAWA, waliokutana na waandishi wa habari makao makuu ya CUF, Buguruni, jijini Dar es Salaam na kutangaza kumkaribisha Edward Lowassa ndani ya vyama vyao.

Wenyeviti wengine walikuwa James Mbatia, NCCR- Mageuzi; Emmanuel Makaidi, National League Democrat (NLD); na Freeman Mbowe, Chadema.

Prof. Lipumba ndiye aliyetoa tamko la kumkaribisha Lowassa kujiunga na UKAWA ili kutimiza adhima yao ya kukiondoa CCM madarakani.

Tayari Lowassa amejiunga na Chadema na kutangazwa kuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Naye Juma Duni Haji, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa CUF, ametangazwa kuwa mgombea mwenza, baada ya kutimiza takwa la kikatiba la kujiuzulu nyazifa zake na kujiunga na Chadema.

Kabla na baada ya Lowassa kujiunga na upinzani kumekuwa na vishawishi vingi vinavyowataka viongozi wakuu wa UKAWA kumzuia Lowassa kujiunga na umoja huo.

Taarifa zinasema, Lowassa mwenyewe alikuwa akishawishiwa kupitia watu mbalimbali waliotumwa na viongozi wa CCM, serikali, madhehebu ya dini na marafiki zake, kutokihama chama chake alimojiunga moja kwa moja alipotoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kukulia humo.

Hata hivyo, Lowassa alilazimika kusema, kimoyomoyo, na baadaye wazi na kwa sauti, akikariri kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alipoona chama chake kinakwenda kuzimu, kuwa “CCM siyo baba wala mama!”

Taarifa zimesema kumekuwa na shinikizo kadhaa kutoka serikalini, CCM na ndani ya familia yake; zikitaka mwanasiasa huyo kutohama chama chake

Miongoni mwa waliokuwa wanahaha kumzuia Lowassa kuondoka CCM, ni pamoja na swahiba wake wa karibu, Rostam Aziz; mfanyabiashara na mmiliki wa kampuni ya kuchapisha magazeti ya New Habari Corporation.

Wengine waliotajwa kumpelekea ujumbe katika sura mbalimbali – ombi, ushawishi, shinikizo – ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana; Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mgombea urais wa chama hicho, John Magufuli na baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Huku kukiwa na ushawishi Lowassa asitoke CCM, upande mwingine kulikuwa na ushawishi kwa Chadema – ukitafuta viongozi wa chama hicho kukataa kumpokea Lowassa.

Miongoni mwa wanaodaiwa kutumiwa na baadhi ya viongozi ndani ya CCM na TISS, kumzuia Lowassa kujiunga na Chadema, ni pamoja na Josephine Mushumbuzi, mke wa Dk. Willibrod Slaa.

“Hilo la Josephine linaeleweka,” ameeleza kiongozi mmoja wa CCM aliyejiapiza kuhamia Chadema na kuongeza, “Anaona nafasi yake ya ‘Festiledi’ (mke wa rais) – inahamia kwingine.”

Lowassa, ambaye alijiunga na Chadema wiki mbili zilizopita, alikuwa miongoni mwa wagombea 38 wa urais waliojitosa katika kinyang’anyiro cha urais kupitia CCM. Jina lake liliondolewa katika hatua za awali; na yeye amekuwa akilalamika kuwa ilikuwa kinyume cha kanuni, taratibu na katiba ya chama hicho.

Alitajwa kuwa mmoja wa wanasiasa wenye ufuasi mkubwa ndani ya CCM kutokana na kubeba kundi kubwa la wafuasi analodaiwa kuunda kwa juhudi binafsi na kukuza kwa ushabiki wa viongozi na wanachama.

Kupatikana kwa taarifa kuwa safari ya Lowassa ya kujivua “kijani” na kujiunga na chama cha magwanda – Chadema, ilikuwa ngumu – mithili ya kuvuka mito, kupanda milima na kushuka mabonde – kumekuja siku moja baada ya mwanasiasa huyo kutangaza kuhama chama chake.

“Haikuwa kazi rahisi Lowassa kuhama CCM na kujiunga na Chadema. Tulilazimika kufanya kazi kubwa na ya ziada kuzuia shinikizo za kutaka asiondoke,” ameeleza mmoja wa walio karibu na Lowassa na Chadema.

Habari zinasema, Rostam alifanya kazi usiku na mchana kujaribu kumzuia Lowassa kuondoka CCM; lakini juhudi zake hazikufanikiwa kwa kuwa, baada ya Lowassa kuweka msimamo wa kuondoka, aliamua kuwaficha taarifa muhimu baadhi ya marafiki zake.

error: Content is protected !!