September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba aendelea kung’oa vigogo CUF

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, ameendelea kufanya mabadiliko madogo ya uongozi wa chama hicho, kwa kutengua uteuzi wa manaibu wakurugenzi wawili na viongozi wa Jumuiya ya Vijana ( JUVICUF). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa ya utenguzi huo imetolewa leo Alhamisi, tarehe 9 Septemba 2021 na Prof. Lipumba, siku 17 tangu alipofanya mabadiliko ya uongozi wa CUF.

Kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa umma, Prof. Lipumba amesema amechukua hatua hiyo, kwa kuzingatia midhamu ya chama hicho.

Katika mabadiliko hayo, Prof. Lipumba ametengua uteuzi wa Mohamed Vuai Makame, katika nafasi ya Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi CUF, pamoja na kumng’oa Khamis Mohamed Faki, katika nafasi ya Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, wa chama hicho.

“Kwa kuzingatia hali ya kisiasa na nidhamu ndani ya Chama, leo tarehe 09 Septemba 2021, natengua uteuzi wa Makame katika nafasi ya Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi. Pia natengua uteuzi wa Faki kuwa Naibu Mkurugenzi Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma,” imesema taarifa ya Prof. Lipumba.

Vuai ameondolewa katika nafasi hiyo miaka miwili, tangu alipoteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, huku Faki akiondolewa siku 17, tangu alipoteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari CUF, tarehe 23 Agosti 2021.

“Tarehe 28 Aprili 2019, nilimteua Makame kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi na alithibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa. Tarehe 23 Agosti 2021, nilimteua Faki kuwa Naibu Mkurugenzi Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma lakini alikuwa bado hajathibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa,” imesema taarifa ya Prof. Lipumba.

Mbali na utenguzi wa manaibu wakurugenzi hao, Prof. Lipumba ametengua uteuzi wa Hamidu Bobali, katika nafasi ya Kaimu Mwenyekiti wa JUVICUF, na wa Chande Jidawi, kwenye nafasi ya Naibu Katibu wa jumuiya hiyo. Viongozi hao aliwateua tarehe 28 Aprili 2019.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa nidhamu ndani ya Chama na kuwa na viongozi watakao jitolea kujenga Jumuiya ya Vijana, leo tarehe 09 Septemba 2021, natengua uteuzi wa Hamidu Bobali wa Kaimu Mwenyekiti na Chande Jidawi, wa Kaimu Naibu Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa CUF,” imesema taarifa ya Prof. Lipumba.

Taarifa hiyo imesema, nafasi zilizoachwa wazi kupitia mabadiliko hayo zitajazwa baadae “uteuzi wa kujaza nafasi hizi utafanyika baadaye.”

error: Content is protected !!