October 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Kahigi ahoji huduma za afya

Maboski ya dawa za binadamu

Spread the love

MBUNGE wa Bukombe, Prof. Kulikoyela Kahigi (Chadema), amesema kitendo cha Serikali kulimbikiza deni la Bohari Kuu ya Madawa (MSD), kimesababisha huduma za afya kwa akina mama na watoto chini ya miaka mitano na wazee kuwa kiini macho. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Prof. Kahigi ametoa kauli hiyo bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza na kuitaka serikali ieleze ni lini italipa deni hilo ili huduma za afya ziweze kupatikana kwa walengwa hao.

Kwa mujibu wa Prof. Kahigi, kwa sasa serikali inadaiwa na MSD zaidi ya Sh. 100 milioni lakini deni hilo halijalipwa.

“Pamoja na serikali kujinadi kuwa inatoa elimu bure kwa wazee, akina mama na watoto chini ya miaka mitano lakini hali imekuwa tofauti na maneno ya serikali. Watu hao wanapotakiwa kwenda kupata matibabu wanajikuta wanakosa huduma katika vituo va afya na badala yake wanakuja kwetu wabunge ili tuwasaidie na tunawasaidia kwa njia moja au nyingine.

“Na huduma hizo zimekuwa kiini macho kwa jamii hizo, je ni lini serikali itaweza kulipa deni hilo ili wananchi waweze kupata matibabu yenye uhakika kwani kwa sasa wanapoenda katika vituo vya afya wanaambiwa wanunue dawa wenyewe,” amehoji.

Awali, katika swali la msingi la mbunge huyo, alitaka kujua serikali imejipangaje katika kutekeleza sera ya huduma bure kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee na watu wenye ulemavu.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Afya na Usawi wa Jamii, Dk. Seif  Rashidi, amesema kuwa sio kweli kuwa MSD inaidai serikali bali serikali imekuwa ikiwekeza zaidi katika bohari hiyo.

Kwamba, kuwa pamoja na juhudi za serikali kutoa huduma bure bado kuna changamoto nyingi. Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pomoja na wagonjwa kuongezeka na kusababisha kukosekana kwa dawa katika vituo vya kutolea huduma.

Ameongeza kuwa ufinyu wa bajeti katika sekta ya afya unachangia kwa kiasi kikubwa kutowapatia huduma bora walengwa hao kama sera inavyotakiwa kutekelezwa.

error: Content is protected !!