PROFESA Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amejigamba kwamba, kwenye nchi hii amefanya kazi ya kutukuka na kuwa, anayemchukia na kumwonea wivu, amchukie tu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
“Anayemchukia Kabudi na aendelee kumchukia, anayempinga na aendelee kumpinga, lakini Kabudi atabaki yule yule siku zote,” alisema.
Prof. Kabudi ambaye kitaaluma ni mwanasheria mbobezi alitoa kauli hiyo tarehe 30 Mei 2019 bungeni wakati akijibu hoja za wabunge katika mjadala wa bajeti ya wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2019/20.
Waziri huyo amesema kuwa, hatishwi wala kusononeshwa na wale wanaomtakia mabaya kwenye kazi yake na kuwa, uzalendo wake kwa taifa hili ni mkubwa na usiotiliwa shaka yoyote.
Akionekana kujibu mapigo kwa wale wanaombeza bila kuwataja, Prof. Kabudi alisema kuwa, yeye alisajiliwa katika dirisha dogo hivyo anayendelea kupiga hazi bila kuyumbishwa na watu wasiompenda ama kumtakia mema.
Prof. Kabudi aliwaeleza wabunge baadhi ya kazi alizozifanya kwa maslahi ya taifa, ikiwa ni pamoja na kuandaa na kuandika Sheria ya Mazingira ambayo inatumika mpaka hii leo.
Pia alieleza kuwa, ndiye aliyefanya kazi ya upatanishi kwa wabunge wa upinzani wakati huo, Hamad Rashidi Mohamed na Dk Wilbrod Slaa wakati wa kutunga sheria ya kupambana na rushwa.
Wakati akitoa kauli hiyo, alisoma Hansard (kumbukumbu rasmi) za Bunge zilizomtaja kwa wakati huo ili kuthibitisha kauli yake.
Leave a comment