Thursday , 18 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Kabudi azidi kung’ang’aniwa
Habari za SiasaTangulizi

Prof. Kabudi azidi kung’ang’aniwa

Spread the love
KAMPUNI ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), wachapishaji wa magazeti ya MwanaHALISI, MSETO na MAWIO, imemshukia Prof. Palamagamba Kabudi, kufuatia kauli yake, kwamba “serikali ya Rais John Pombe Magufuli, haibani uhuru wa habari nchini. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo kwa vyombo vya habari, leo Jumamosi, tarehe 13 Julai 2019, inaeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Prof. Kabudi, kuudanganya ulimwengu, kuwa nchini Tanzania, kuna uhuru mkubwa wa waandishi wa habari na vyombo vyao.

“Kwa ajili ya kumkumbusha Waziri Prof. Kabudi na kuusaidia umma mpana ambao waweza kuwa umepotoshwa na matamshi ya waziri huyu wakati akihojiwa na BBC, tunapenda kuweka kumbukumbu sawa.

“Kwamba nchini Tanzania, kuna magazeti matatu, ambayo yamesajiliwa kutoka kila wiki (MSETO, MAWIO na MwanaHALISI). Magazeti haya uchapishaji na usambazaji wake umesitishwa na serikali, kati ya miaka miwili na miaka mitatu.”

Prof. Kabudi alitoa kauli hiyo, tarehe 10 Julai 2019, wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha BBC nchini Uingereza. Alikuwa akijibu swali juu ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania.

Katika mahojiano hayo, Prof. Kabudi alinukuliwa akisema hajui gazeti lolote ambalo uchapishaji wake umewahi kusimamishwa na serikali, isipokuwa gazeti la The Citizen, ambalo lilisimamishwa kwa muda wa siku saba.

“Magazeti ya MwanaHALISI na MAWIO ambayo uchapishwaji na usambazwaji wake vilisimamishwa na serikali mwaka 2017, bado hayajaruhusiwa kuingia tena mitaani, pamoja na kuwa yameshinda kesi mahakamani na pengine kumaliza adhabu.

“Tunamfahamisha waziri huyu kuwa mpaka sasa, gazeti la MSETO ambalo uchapishwaji na usambazaji wake vilisimamishwa na serikali mwaka 2016 bado halijaruhusiwa kuingia mitaani.”

Aidha, kampuni hiyo inasema, wakati akihojiwa na kituo cha habari cha BBC, Waziri Prof. Kabudi alisema, magazeti ambayo uchapishwaji na usambazwaji wake umesitishwa na serikali, “yanaweza kutafuta nafuu ya kisheria kutoka kwa waziri wa habari.

“Hapa  tunapenda pia kumfahamisha Waziri Kabudi kwamba, ukweli ni kuwa hakuna uwezekano huo. Waziri wa Habari ndiye ambaye hufanya uamuzi wa kusimamisha uchapishwaji na usambazwaji wa magazeti nchini na bila kutoa fursa kwa wamiliki wa magazeti hayo kujitetea,” inaeleza taarifa ya kampuni hiyo inayoendesha pia magazeti ya MwanaHALISI ONLINE na MwanaHALISI TV.

Taarifa ya kampuni hiyo imesainiwa na mkurugenzi wake mtendaji, Saed Kubenea.

Inasema, “tunapenda umma ufahamu kwamba, uongozi wa HHP Limited, uliamua kutafuta nafuu ya kisheria kupitia mahakama zetu, utaratibu ambao ni halali kikatiba; na mahakama ilitoa uamuzi kuwa serikali ilikosea kisheria kusimamisha uchapishwaji na usambazwaji wa magazeti ya MSETO, MwanaHALISI  na MAWIO.

“Mahakama ikatoa amri kwamba magazeti haya yapatiwe kibali cha kuendelea kuchapishwa na kusambazwa bila mashari yoyote. Hata hivyo, mpaka leo hii (jana), tarehe 12 Julai 2019, serikali haijatoa leseni ya uchapishaji na usambazaji wa magazeti haya.”

Katika kuweka msisitizo wa hoja yake, HHPL imetoa inachoita, “mtiririko wa ufafanuzi, kwa lengo la kutoa mwanga mpana kuhusu mvutano kati yake na serikali na madhara ya hali ngumu inayoikabili kampuni ya HHPL katika harakati zake za kuyarejesha magazeti yake matatu mtaani ili kuwanusuru wafanyakazi wake dhidi ya ukata unaowafanya kushindwa kujikimu.”

Inasema, “mnamo tarehe 26 na 27 Julai 2012, lilitolewa tangazo kupitia Gazeti la Serikali, Toleo Na. 258 la tarehe 27 Julai 2012, likiwa limebeba amri ya serikali ya kusimamisha uchapishwaji na usambazwaji wa gazeti la MwanaHALISI.

“Kwamba, mnamo tarehe 30 Julai 2012, Msajili wa Magazeti aliuandikia barua uongozi wa HHPL kuujulisha kwamba serikali ilikuwa tayari imefanya uamuzi wa kulifunga gazeti la MwanaHALISI i kwa muda usiojulikana.

“Kutokana na kutoridhishwa na uamuzi wa serikali uongozi wa HHPL alifungua kesi Na. 27 ya mwaka 2013 katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Masjala ya Dar es Salaam), kwa ajili ya kuomba mapitio ya kisheria. HHPL ilihoji uhalali wa uamuzi wa serikali kulifunga gazeti kwa muda usiojulikana.

“Kwa sababu ya serikali kushindwa kutuma mwakilishi wake mahakamani kusikiliza shauri hilo, Mahakama Kuu iliamua kuendelea mbele kwa kusikiliza upande mmoja wa mleta maombi.

“Hatimaye Mahakama ilikubaliana na maombi yote ya HHPL tuliyoyawasilisha kupitia chemba samansi; ombi kuu likiwa ni madai kwamba, Mahakama Kuu itupilie mbali amri ya serikali iliyotolewa kupitia gazeti la Serikali, toleo Na.258 la tarehe 27 Julai 2012 dhidi ya gazeti la MwanaHALISI.

“Baada ya hukumu hii, serikali ilitangaza nia ya kukata rufaa na rufaa hiyo ilisajiliwa kwa kupewa Na. 13 ya 2016. Rufaa ya serikali ilikuwa inapinga uamuzi wa Mahakama Kuu. Siku ya kusikiliza rufaa hii ilipofika, Oktoba mwaka 2016, serikali iliomba kesi iahirishwe ili iweze kupata fursa ya kusajili hoja mpya kuhusiana na kesi hii. Kesi iliahirishwa.

“Lakini wakati huo huo tayari HHPL tulikuwa tumekwisha sajili mapingamizi ya awali mawili kuhoji uhalali wa rufaa iliyosajiliwa na serikali.

“Katika mapingamizi haya, hoja yetu ya msingi ilikuwa kwamba, kwa kuwa uamuzi wa Mahakama uliotolewa kwa kusikiliza upande mmoja unaweza kukatiwa rufaa baada ya kusajiliwa kwa maombi ya kutenguliwa kwa uamuzi huo, na kwa kuwa serikali ilikuwa imekata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama uliotolewa kwa kusikiliza upande mmoja kabla ya kusajiliwa kwa maombi ya kutenguliwa kwa uamuzi huo, basi, inafuata kimantiki kwamba, rufaa iliyosajiliwa na serikali ilikuwa batili kisheria.

“Rufaa tajwa ilisikilizwa tena tarehe 14 Mei 2019,  lakini kwa sababu ambazo hazijulikani kwa uongozi wa HHPL na uongozi wa Mahakama, mwakilishi wa serikali hakutokea mahakamani.

Katika mazingira haya, wakili wa HHPL aliiomba Mahakama chini ya Kifungu cha 106(17) cha Kanuni za Mahakama ya Rufaa za mwaka 2009, kufuta rufaa husika. Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na ombo hili na kuifuta rufaa hiyo inayolihusu gazeti la MwanaHALISI.”

Akizungumzia mvutano kuhusu gazeti la MSETO, taarifa ya kampuni inasema, “mnamo Oktoba 2016, uongozi wa HHPL ulikwenda katika Mahakama ya Afrika Mashariki ( EACJ) na kusajili maombi ya kupinga kufungwa kwa gazeti lake la MSETO. Mawakili wetu walijenga hoja kwamba, uamuzi wa serikali ulikuwa unakiuka vifungu vya Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tarehe 21 Juni 2018, Mahakama ya Afrika Mashariki yenye makao makuu yake jijini Arusha nchini Tanzania, ilitoa uamuzi wake na kukubaliana na hoja zetu. Serikali ya Tanzania ilitangaza nia ya kukata rufaa kupitia maombi Na. 03 ya mwaka 2018 yaliyosajiliwa katika Mahakama ya Afrika Mashariki.

“Tangu Juni 2018 mpaka 13 Mei 2019, serikali ya Tanzania haikuchukua hatua yoyote kwa ajili ya kusajili rufaa husika. Uchelewaji huu uliwafanya mawakili wa HHPL kusaili maombi Na. 03 ya mwaka 2019, katika Divisheni ya Rufaa ya Mahakama ya Afrika Mashariki, wakiomba kufutwa kwa maombi ya serikali namba 03 ya mwaka 2018.

“Matarajio yetu ni kwamba mvutano huu kati ya serikali na HHPL juu ya gazeti la MSETO utaishia katika hatua hii.”

Vilevile, kampuni imeeleza mvutano wa Pili kuhusu gazeti la MwanaHALISI, kwamba “mnamo tarehe 19 Septemba 2017, serikali ilidai kwamba, kwa mujibu wa staili ya uandishi na maudhi ya makala kadhaa ya gazeti la MwanaHALISI, waziri wa habari aliona kuwa gazeti lilikuwa linakiuka maadili ya uandishi wa habari.

“Mhariri wa gazeti alitakiwa, ndani ya muda wa saa mbili, kueleza kwa nini gazeti lisichukuliwe hatua za kinidhamu. Mhariri alifanya hivyo na kufanikiwa kujibu kwa ufasaha tuhuma zote dhidi ya gazeti akipinga dhana kwamba gazeti lilikuwa limekiuka maadili ya uandishi wa habari na sheria za nchi.

“Pamoja na majibu mazuri ya mhariri, serikali ililisimamisha tena gazeti la MwanaHALISI kupitia barua yenye Kumb. Na. IH/RN/750/103. Barua inaamuru kwamba gazeti litakapofunguliwa linapaswa kusajiliwa upya.

“Hatukukubaliana na uamuzi wa serikali. Hivyo, mnamo 20 Novemba 2017 tulisajili mamobi namba 90 ya mwaka 2017 kutafuta ruhusa ya kimahakama kwa ajili ya kuishitaki serikali. Tulipewa ruhusa hiyo tarehe 02 Februari 2018 kupitia kwa Jaji I.P. Kitusi, aliyeturuhusu kusajili kesi dhidi ya serikali ndani ya siku 30.

“Mnamo 14 Februari 2018 tulisajili madai Na 02 ya mwaka 2018. Maombi haya yalisikilizwa kwa njia ya maandishi. Hukumu ya mahakama ilitolewa 24 Julai 2018 kupitia kwa Jaji Mtungi na kutupa ushindi.

“Mara tu baada ya hukumu hii, tarehe 09 Agosti 2018, mawakilishi wa serikali kupitia barua yenye Kumb. Na. AGC/Misc/MARCH/2018/10/22 iliwasilisha Mahakama Kuu maombi ya kupatiwa kumbukumbu za mwenendo wa kesi, hukumu, amri ya mahakama, vilelezo, na kibali cha kumruhusu kuchelewa kusajili kesi ya rufaa kama ikitokea akachelewa.

“Naye Msajili wa Mahakama, kupitia barua Na. Misc./CIVIL C./NO.02/2018 aliifahamisha serikali kwamba, kumbukumbu zilizoombwa zilikuwa tayari. Kwa mujibu wa taratibu za kimahakama, serikali ilipaswa kusajili kesi ya rufaa katika Mahakama ya Rufaa ndani ya siku 30 tangu hukumu husika ilipotolewa. Serikali haikufanya hivyo.

“Baada ya kuona kwamba, serikali ilikuwa imeshindwa kutekeleza nia yake ya kukata rufaa ndani ya siku 30, HHPL imelisajili notisi ya kuikumbusha Mahakama. Mpaka tarehe tuliposajili notisi hii, serikali haikuwa imesajili Mahakamani randama ya Rufaa, kitendo ambacho walipaswa kukifanya ndani ya siku 60 tangu siku walipofahamishwa na Msajili wa Mahakama kuwa nyaraka walizoomba zilikuwa tayari.

“Kutokana na mazingira haya HHPL tunaanza kuamini kwamba serikali imetupilia mbali dhamira yake ya kukata rufaa. Kwa hiyo, mtu anaweza kushangaa ni kwa nini serikali ilikuwa imetangaza nia ya kukataa rufaa hapo awali. Ni mtazamo wetu kwamba, serikali ilikuwa na nia ya kutusababishia maumivu ya kiuchumi kwa kutuondolea fursa ya kuzalisha na kusambaza gazeti.”

Akizungumzia mvutano wa gazeti la MAWIO, Kubenea amesema,  “tunamkumbusha Waziri Kabudi, kwamba gazeti la MAWIO lilisimamishwa na serikali kwa miezi 24 tangu 15 Juni 2015 mpaka 14 Juni 2019. Mhariri na mmiliki wa MAWIO walifanikiwa kupinga uamuzi wa serikali Mahakamani.

“Kwamba, tarehe 13 Desemba 2018, Jaji Masoud aliamuru kwamba gazeti hili lilionewa kwa kufungwa bila kutoa nafasi ya kusikilizwa ka mmiliki wake, jambo ambalo ni kinyume cha haki asilia. Bahati nzuri, serikali haikukata rufaa safari hii.

“Kwa sababu hii, Victoria Media Services, ambaye ni Mchapishaji wa MAWIO aliomba leseni, kwa mujibu wa sheria, ili aanze kuzalisha upya gazeti hili. Nyaraka zote ziliwasilishwa kwa msajili wa magazeti tangu 28 Desemba 2018.

“Tarahe 16 Aprili 2019 barua ya kumkumbusha msajili wa magazeti iliandikwa na kuwasilishwa kwake. Hata hivyo, mpaka leo miezi nane baada ya barua ya kwanza kuwasilishwa kwake, Msajili wa Magazeti hajawezi hata kujibu barua zetu.”

Akizungumzia ni kipi kifanyike, kampuni hiyo inasema, “kutokana na machungu haya yote, uongozi wa HHPL unapenda kutoa wito kwa serikali kuheshimu maamuzi ya Mahakama na hivyo kuruhusu magazeti ya MwanaHALISI, MSETO na MAWIO kurejea mitaani kwa faida ya umma mpana wa Watanzania na wafanyakazi wa HHPL wanaoteseka kiuchumi kwa muda mrefu sasa.

“Ni Imani yetu, Prof. Palamagamba Kabudi, waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa, ambaye pengine alikuwa hayajui haya, atasaidia kuhakikisha magazeti hayo yanarejea mtaani, haraka iwezekanavyo,” inaeleza taarifa ya kampuni hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!