July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Juma, Dk. Hoseah wataka Kingereza ‘kisitoswe’ kimahakamani

Spread the love

 

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Dk. Edward Hoseah, wamewashauri mawakili na wanasheria nchini, wasiache matumizi ya lugha ya Kingereza katika shughuli zao, kwa kuwa ni ya kibiashara. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Viongozi hao wametoa wito huo leo Ijumaa, tarehe 9 Julai 2021, katika hafla ya uapisho wa mawakili wapya, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Prof. Juma amesema, ujuzi wa mawasiliano huongeza sifa na vigezo kwa mawakili, katika kushindana kwenye soko la ajira.

“Sifa gani au ujuzi gani mnatakiwa kuwa nao ili muweze kushindana, ni pamoja na ujuzi wa mawasiliano. Kuwasiliana kwa lugha, lugha ya Kiswahili na Kingereza,” amesema Prof. Juma na kuongeza:

https://youtu.be/nsnO3S9pdRc

“Kingereza ni muhimu sana sababu ni lugha ya biashara na uwekezaji, Kiswahili lazima ukifahamu sababu lugha ya Watanzania wenzako.”

Kwa upande wake Dk. Hoseah, amesema Kingereza hakipaswi kuacha kutumika katika shughuli za kisheria, kwa kuwa ni lugha ya kibiashara kwa mawakili.

“Tusijidanganye kwamba Kingereza hakina nafasi, ni lugha ambayo Taifa tunaihitaji tuweze kufanya biashara duniani. Lugha ni muhimu,” amesema Dk. Hoseah.

Dk. Hoseah ameishauri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, iweke mkazo katika kufundisha wanafunzi lugha ya Kingereza na Kiswahili.

“Pengine tutafakari tunavyofundisha watoto wetu kutoka shule ya msingi, hadi vyuo vikuu. Je, tunawapa mafundisho mazuri ya kutawala lugha? Iwe Kiswahili, iwe yoyote,” amesema Dk. Hoseah na kuongeza:

“Kwa hivyo, huo ndiyo msisitizo wangu, hatujachelewa kama Taifa turudi kwenye misingi ya lugha. Tuzitizame tuone namna gani zitatusaidia kupiga hatua kama taifa.”

Wito huo umetolewa wakati Tanzania ikiwa katika mchakato wa mabadiliko ya sheria, ili kukiwezesha Kiswahili kuwa lugha rasmi katika shughuli za kimahakama.

Mchakato huo ulianza baada ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, kuagiza Mahakama iweke mkakati wa Kiswahili kutumika katika shughuli zake.

Magufuli alitoa agizo hilo mwezi mmoja kabla hajafariki dunia akiwa madarakani, tarehe 17 Machi 2021, ambapo alisema matumizi ya Kingereza katika shughuli za mahakama inanyima wananchi haki.

Pia, inawaongezea gharama kupitia ukalimani wa kutafsiri hukumu na mienendo ya kesi zao.

Mwili wa Magufuli aliyeiongoza Tanzania kwa muda wa miaka mitano na miezi mitano mfululizo (Novemba 2015-Machi 2021), ulizikwa nyumbani kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi mwaka huu.

error: Content is protected !!