January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Baregu: Chadema tuko wamoja

Viongozi wa Juu wa Chadema

Spread the love

PROF. Mwesiga Baregu amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kingali kimoja na sasa imara zaidi.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu (CC) ya Chadema alikuwa akizungumzia mjadala mkali ndani ya chama na katika mitandao na vyombo vya habari juu ya Edward Lowassa kuhama CCM na kujiunga na chama chake.

“Ni kweli, kulikuwa na mjadala mkali ndani ya chama, juu ya kumpokea Lowassa. Kulikuwa na pande mbili. Wapo waliotaka Lowassa apokelewe na wapo waliopinga. Lakini mwishoni wote tulikubaliana kwa kauli moja, kwamba tunamkaribisha,” anaeleza Prof. Baregu.

Anasema, “…wala hilo siyo jambo la ajabu. Suala lililokuwa mbele yetu lilikuwa kubwa na lilihitaji mjadala wa kina. Sisi ni watu wazima, hatuwezi kukimbilia mambo. Ni lazima tufanye utafiti wa kupima hasara na faida ya kile tunachotaka kufanya.”

Prof. Baregu alikuwa akijibu madai kuwa ndani ya Chadema kumeibuka mpasuko unaotokana na hatua ya viongozi wake wakuu, wakiongozwa na mwenyekiti Freeman Mbowe, kumkaribisha Lowassa ndani ya chama hicho.

Prof. Baregu, anatajwa kuwa ni miongoni mwa viongozi waliopinga Lowassa kujiunga na Chadema. Wengine waliopinga, ni Dk. Willibrod Slaa, Tundu Lissu na John Mnyika.

“Katika hili, nilikuwa na hofu mbili,” anaeleza Prof. Baregu. Anasema, “…kwanza, ni kuhusu tuhuma za ufisadi ambazo Lowassa alikuwa anatuhumiwa nazo; na pili, nilitaka kujiridhisha ikiwa mafuriko anayokuja nayo, hayataweza kukikumba chama na kukifanya kipoteza ile mbegu yake ya asili.”

Lowassa alitangaza kujiuzulu uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), juzi Jumanne jijini Dar es Saalam. Muda mfupi baadaye akajiunga na Chadema.

Taarifa zinasema, mjadala kuhusu haja ya kumpokea Lowassa na baadaye kumfanya kuwa mgombea urais wa vyama vya upinzani chini ya mwavuli wa UKAWA, ulipamba moto katika vikao kadhaa, vikiwamo vile vya mashauriano vilivyofanyika jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Prof. Baregu amesema, “…lakini baada ya mjadala mpana na ufafanuzi yakinifu tulioupata, kila mmoja akajiridhisha kuwa Lowassa aruhusiwe kujiunga na chama chetu.”

Anasema, “Hivyo basi, haya yote yaliyofanyika ya kumpokea Lowassa na baadaye ikibidi hata kumteua kuwa mgombea wetu wa urais, yamepitia vikao halali vya chama na uamuzi uliofikiwa umepatikana kwa baraka za viongozi wote kwa ngazi husika.”

Taarifa zinasema, mjadala huo uliibuka tena katika kikao cha kamati kuu, kilichofanyika Jumapili iliyopita, baada ya Mbowe kuripoti ujio wa Lowassa ndani ya chama hicho. Aliyeongoza upinzani safari hii, alikuwa Lissu ambaye alisaidiwa na Dk. Slaa.

Taarifa zinasema, Lissu na Dk. Slaa, walisimamia hoja kuwa mbunge huyo wa zamani wa Monduli, ni miongoni mwa watu 11 waliowatangaza kwenye mkutano wa hadhara, Septemba mwaka 2007, kuwa ni watuhumiwa wa ufisadi.

Lakini mtoa taarifa anasema, hoja za Lissu na Dk. Slaa zilizimwa na baadhi ya wajumbe, kwa maelezo kuwa kinachotajwa ni tuhuma na kwamba bado hazijathibitishwa.

“Mle ndani ya kamati kuu, mjadala ulikuwa mkali sana. Lakini baada ya kutolewa ufafanuzi wa kina, kila mmoja aliridhika na kuamuliwa Lowassa kuruhusiwa usiku wa siku hiyo, kuingia katika kikao hicho,” anaeleza mmoja wa viongozi wa Chadema.

Anasema, baada ya Lowassa kuingia kwenye kikao hicho na wajumbe kupata maelezo kuhusu madai ya ufisadi katika mkataba tata wa kufua umeme wa Richmond na kinachoitwa, “utajiri wa Lowassa,” wajumbe walipitisha kwa kauli moja, “azimio la kumpokea Lowassa ndani ya Chadema.”

Taarifa kutoka ndani ya CC zinasema, mara baada ya Mbowe kueleza hatua kwa hatua kuhusu ujio wa Lowassa ndani ya chama chake, mmoja wa wajumbe aliomba Lissu na Dk. Slaa kueleza sababu zinazowafanya kugomea jambo hilo.

Inaelezwa baada ya viongozi hao wawili kuwasilisha hoja zao kwa kina na wajumbe kupata nafasi ya kuchagia, kila mmoja aliridhika. Lissu alifika mbali zaidi kwa kuomba radhi kamati kuu na viongozi wenzake akisema, “taarifa nyingi nimezipata ndani ya kikao.”

Naye Dk. Slaa alinukuliwa akiomba radhi mwenyekiti Mbowe na kamati kuu kwa kile alichoeleza kuwa ni “kumchanganya mwenyekiti” wake. Aliomba radhi kamati kuu na kuridhia Lowassa kujiunga na chama chake.

Mmoja wa wajumbe wa kamati kuu ya Chadema anasema, Lowassa aliwakosha wajumbe kutokana na jinsi alivyojenga hoja na kujibu maswali juu ya masuala hayo mawili kwa kina na kwa ufasaha.

Alisema, “…mikono yangu ni misafi kuhusu suala hili. Yeyote mwenye ushahidi na aende mahakamani.” Alisema kama angekuwa mchafu wala asingefika mbele ya kamati kuu kuomba kujiunga na chama hicho.

“Ningekuwa mchafu, kama ambavyo inaelezwa na wasionitakia mema, wala nisingefika hapa. Lakini nimefika hapa kwa kuwa mimi ni mtu safi. Hakuna ninachokificha.”

Madai kuwa alihusika na mkataba tata wa Richmond, yaliibuka tena katika mkutano wake na waandishi wa habari juzi Jumanne.

Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari, Lowassa alisema, “…anayenichafua kuhusu hili alete ushahidi wake. Kama si hivyo, anyamaze.”

Akiongea kwa kujiamini, Lowassa alisema, alipata taarifa ya udhaifu wa kampuni hiyo kupitia vyombo vya habari; aliitisha kikao maalum cha kamati ya ufundi, ambacho kiliwashirikisha katibu mkuu kiongozi na viongozi wengine wa wizara ya nishati na madini.

Alisema, “…nilitaka kuvunja mkataba. Lakini katibu mkuu kiongozi (Philemon Luhanjo), alitaka kuwasiliana kwanza na mamlaka ya juu. Baadaye akarejea na ujumbe kutoka kwa Rais Kikwete kuwa suala hilo liachwe atalishughulikia.”

Sakata la Richmond ndilo lilisababisha Lowassa kujuzulu wadhifa wake wa waziri mkuu, Februari 2008.

Lowassa amewahi kunukuliwa akisema kwenye vikao vya ndani vya CCM kuwa hakuna alichofanya ambacho rais wake hakujua.

error: Content is protected !!