Tuesday , 16 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Assad: Spika Ndugai aheshimu Katiba ya Nchi
Habari za SiasaTangulizi

Prof. Assad: Spika Ndugai aheshimu Katiba ya Nchi

Prof. Mussa Assad, Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Picha ndogo Job Ndugai, Spika wa Bunge
Spread the love
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Asaad, “amemvua nguo” Spika wa Bunge la Jamhuri, Job Ndugai. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akijibu madai kuwa amelidharau na kudhalilisha Bunge, Prof. Asaad amesema, “ni vema Spika Ndugai akawa mfano bora wa kuheshimu, kuilinda na kuitetea Katiba ya Nchi.”

Kauli ya Prof. Asaad imekuja siku mbili baada ya Spika Ndugai, kuzungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na kumtuhumu kiongozi huyo, kudhalilisha Bunge.

Spika Ndugai alikuwa akirejea kauli ya CAG, aliyoitoa nchini Marekani wiki iliyopita, kwamba mhimili huo wa kutunga sheria, umekuwa dhaifu mno na hivyo umeshindwa kutimiza wajibu wake.

Ndugai alitumia mkutano huo, pamoja na mengine, kuagiza Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, kumhoji Prof. Asaad na baadaye kumshauri yeye hatua za kuchukua.

Akizungumza kwa hasira, Jumatatu iliyopita, mjini Dodoma, Ndugai alisema, Prof. Assad, anatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo, tarehe 21 Januari 2019, ili kujibu “tuhuma za kudhalilisha Bunge.”

Amedai kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa CAG ameliita “Bunge dhaifu.”

Amesema, “…ninamtaka CAG, kufika mbele ya Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, kwa hiari yake, tarehe 21 Januari mwaka huu. Vinginevyo, nitaagiza akamatwe na kuletwa mbele ya kamati kwa pingu.”

Akijibu madai hayo na iwapo ataitikia wito wa Spika Ndugai ama atagomea, Prof. Asaad anasema, “umeuliza kama nitaitikia wito, sitajibu hilo. Ila naomba niweke rekodi sawa; ule siyo wito. Ni amri.”

Anasema, “…sasa kwa kuheshimu katiba yetu na kwa kuwa sitaki kuwa miongoni mwa waivunjao katiba, niseme hivi, Ibara ya 18 (a) inampa kila mtu uhuru wa kutoa maoni.

“Hivyo basi, kwangu mimi nachukulia hayo yote, kama mtu kaamua kutoa maoni yake na kuelezea fikra zake.”

Aidha, Prof. Asaad anasema, “jambo la pili, Ibara ya 26 (1), ya Katiba ya Jamhuri, inaelezea wajibu wa kila mtu kufuata na kutii katiba ya nchi.

“Sasa mimi nilidhani, mtu kama spika wa Bunge, alipaswa kuwa mfano bora katika kuhakikisha kuwa Ibara ya 143 ya Katiba, inayonitambua mimi na taasisi ninayoingoza, inaheshimiwa kama inavyostahiki.”

Prof. Asaad anasema, hatayumbishwa na kauli hizo wala vitisho alivyopewa. Bali anasema, “niseme tu, nitasimamia ninachokiamini kitaaluma na kwa uzalendo kwa maslahi mapana ya taifa letu.”

Tangu Ndugai kutoa wito wa kumtaka CAG kufika mbele ya Kamati za Bunge, watu kadhaa akiwamo Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, wamepinga kiongozi huyo kuhojiwa.

Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter, Fatma anasema, “Ndugai amevunja katiba” na kwamba “kanuni za Bunge haziwezi kuwa juu ya Katiba ya Jamhuri.”

Fatma Karume, ni mtoto wa rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume; na mjukuu wa mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya 12 Januari 1964, ambaye alikuja kufanywa kuwa Rais wa Zanzibar na makamu wa rais wa kwanza wa rais wa Jamhuri ya Muungano, Abeid Amani Karume.

Akihoji hicho kinachoitwa, “kudhalilisha Bunge,” Fatma anasema, “…hiyo ni tafsri tu. Hakuna kitu kinachoitwa kudhalilisha Bunge. Tusitumie madaraka yetu kwa maslahi binafsi.”

Anasema, “mpaka sasa, nikiwa mwanasheria niliyebobea, sijaona mamlaka ya Bunge ya kumkataza raia au CAG kuongea. Lakini naendelea kutafuta.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari za Siasa

Rais Samia amfariji mjane wa Musa Abdulrahman

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan leo Jumanne amempa pole Mwanakheri Mussa...

Habari za Siasa

Nape: Wanasiasa, wanahabari, wafanyabiashara mteteeni Samia

Spread the loveWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,...

Habari za Siasa

CAG: TAWA imegawa vibali vya uwindaji bila idhini ya waziri

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!