April 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Assad amjibu Spika Ndugai

Prof. Mussa Assad, aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali

Spread the love

USHAURI wa Job Ndugai, Spika wa Bunge kwamba, Prof. Mussa Assad, Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ‘akaungame’ kwa Rais John Magufuli, umetupwa. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Jana tarehe 14 Machi 2019 mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Spika Ndugai alimshauri Prof. Assad kwenda kwa rais kueleza ‘amekosea’ ili mambo yaendelee kama kawaida.

Hata hivyo, kauli ya Spika Ndugai imejibiwa na Prof. Assad alipozungumza na gazeti moja nchini akisema ‘rejea Katiba.’

Katika mazungumzo hayo mafupi kwa njia ya simu na gazeti hilo Prof. Assad amesema, Katiba ya Jamhuri haimuelekezi kutenda kile kilichoshauriwa na Spika Ndugai kwamba, aende kujieleza kwa Rais Magufuli.

Akizungumza na wanahabari Spika Ndugai alisema, CAG anampa wakati mgumu Rais Magufuli huku akimshauri ajiuzulu.

Alisema, CAG ajiuzulu kwa kuwa, Bunge tayari limepitisha azimio la kutofanya naye kazi na kwamba, hata nchi za nje Bunge likiwa  halina imani na mdhibiti, hang’ang’anii.

 “Azimio la bunge ni halali …katika nchi za wenzetu bunge likiwa halina imani na wewe, hung’ang’ani unajiuzulu. Sisi hatumfundishi lakini anampa wakati mgumu Rais.

“ . ..aende kwa rais amueleze rais kwamba, aliteleza ..matusi hayo anayoyatoa kwa Bunge anamtukana kila mtu, rais yupo mule,Waziri mkuu yumo mule, Baraza la mawaziri wapo mule anautukana hadi mkono unaomlisha,” alisema Spika Ndugai.

Hata hivyo, Prof. Assad alilieleza gazeti hilo kwamba, Katiba ya Jamhuri haina kifungu kinachomtaka kwenda kujieleza huku akirejea Ibara ya 143 (6).

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri Ibara ya 143 (6) inaeleza; “….Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hatalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu mwingine yoyote ama idara nyingine yoyote ya serikali, lakini maelezo hayo ya ibara hii ndogo hayatazuia mahakama nayo kutumia madaraka yake kwa ajili ya kuchunguza kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ametekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii au sivyo.”

Mgogoro wa Spika Ndugai na Prof. Assad uliibuka baada ya Prof. Assad kutamka kwamba, Bunge ni dhaifu wakati akiwa kwenye mahojiano na Kituo cha Redio ya Umoja wa Kimataifa nchini Marekani mwishoni mwa mwaka jana.

error: Content is protected !!