August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ponda amfuata Lema mahabusu

Spread the love

USIRUDI nyuma, endelea kupigania haki za wananchi wanyonge na hutadhoofu kwa kukaa gerezani, anaandika Faki Sosi.

Ni kauli ya Sheikh Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini aliyomwambia Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini alipomtembelea kwenye mahabasu ya Gereza la Kisongo jijini humo.

Kwenye safari ya kwenda kwenye gereza hilo Sheikh Ponda aliongozana na Noel Ole Varoya, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA).

“Nimemweleza kwamba, hawezi kuwa dhofu kwa kukaa gerezani ama mahabusu. Nimemwambia historia inaeleza wazi kwamba, viongozi wanaowekwa gerezaji wakitoka huwa imara zaidi.

“Natarajia kwamba, akitoka humo ataendelea kuwa imara zaidi, asirudi nyuma kwa kuwa, kurudi kwake nyuma kutaumiza wengi,” amesema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda mara kadhaa amekuwa akikamatwa na kufikishwa mahakamani na hata kutupwa kwenye Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam kwa madai mbalimbali ya uchochezi.

Miongoni mwa madai ya uchochezi ya Jamhuri kwa Sheikh Ponda yalikuwa mwaka 2013.

Mwaka huo Sheikh Ponda alishikiliwa mahabusu na kuachwa huru mwaka 2015 katika Mahakama ya Morogoro baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka yake.

Lema alifikishwa kwenye Mahakama ya Kuu Kanda ya Arusha tarehe 29 Agosti mwaka huu na kusomewa mashtaka mawili;

La kwanza akidaiwa kutuma ujumbe wa kuudhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo unaosema‘karibu Arusha tutakudhibiti kama Arabuni wanavyodhibiti mashoga’.

La pili akidaiwa kutuma ujumbe wa sauti kwenye mitandao unaohamasisha maandamano yasiyokuwa na kibali.

Kwenye kesi hilo Lema anatetewa na John Malya, Peter Kibatala, Faraji Mangula, Adam Jabir na Sheki Mfinanga wakati Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili waandamizi Matrenus Mrandu na Paul Kadushi.

 

error: Content is protected !!