Thursday , 28 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Pombe yazua balaa Z’bar
Habari MchanganyikoTangulizi

Pombe yazua balaa Z’bar

Spread the love

 

BODI ya Wadhamini wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA), imesema imeamua kufungua kesi upya dhidi ya bodi ya vileo Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kutoridhishwa na kufutwa kesi ya awali na Jaji wa Mahakama Kuu, Rabia Hussein Muhammed tarehe 2 Juni 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari makao makuu ya Jumaza Majestic Mjini Zanzibar, Katibu wa Kamati ya Maadili na Baraza la Taasisi ya Kiislamu Zanzibar, Shekhe Abdallah Mnubi Abasi, alisema Mahakama imekwepa kujibu hoja za msingi za kuvunjwa kwa sheria ya vileo namba 9 ya mwaka 2020.

Bwaba Abasi, alisema “kwa mujibu wa kifungu 33(1) kampuni zinazotakiwa kupewa vibali vya kuingiza Pombe mwisho ni tatu lakini bodi imetoa zaidi ya kampuni nane mpaka kufikia Febuari mwaka huu kinyume na sheria”.

Alisema kimsingi masharti ya sheria hiyo, anayepewa kibali lazima awe mzanzibari, awe mlipa kodi, awe na ghala la kuhifadhia vileo pamoja na gari ya kusambazia bidhaa hiyo.

“Kampuni zilizojitokeza baada ya kutangazwa zabuni zilikuwa tatu na ndio zilizopitishwa lakini badala yake kulianza kutolewa vibali vingine kinyemela kinyume na sheria namba 9 ya mwaka 2020,” alisema Shekhe Abasi.

Aidha alisema kifungu cha 28(k) kinasema maduka ya kuuzia pombe na baa lazima yawe umbali wa mita 1,000 kutoka katika maeneo ya huduma za jamii kama Hospital, Nyumba za ibada, madrasa na makaazi ya watu lakini bodi imeshindwa kusimamia masharti hayo.

Aidha alisema kwamba inasikitisha mpaka sasa bodi ya vileo haijachukuliwa hatua yoyote tangu kuanza kuvunjwa kwa sheria na kusababisha mtafaruku katika jamii na viongozi wa taasisi za dini Zanzibar.

“Kitendo cha viongozi wa bodi kuendelea kubaki katika nyazifa zao licha ya sheria kuvunjwa kunaleta picha mbaya dhidi ya serikali na kuvuruga malengo na madhumuni ya kutungwa sheria mpya ya vileo,”alisema.

Alisema kwamba kabla ya sheria kutungwa, ilipitishwa katika vikao vizito vya serikali kuanzia makatibu wakuu, baraza la mawaziri, kabla ya kuwasilishwa mswaada wa sheria Baraza la Wawakilishi na kuanza kutumika baada ya kusainiwa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Muhamed Shein.

Alisema wakati Serikali inaendelea kukabiliana na tatizo la udhalilishaji wa wanawake na watoto lakini imeshindwa kuangalia chimbuko la kuongezeka kwa vitendo hivyo ikiwemo uingizaji holela wa pombe kutokana na sheria kushindwa kusimamiwa.

Awali Jaji Rabia Hussein Muhammed aliifuta kesi iliyofunguliwa na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar kwa madai ya kufunguliwa kinyume na sheria baada ya kuishtaki bodi ya vileo badala ya mwanasheria mkuu wa serikali na kushindwa kutoa indhari ya kuishitaki serikali kwa muda wa siku 60 kabla ya kufungua kesi.

Kwa upande wake, Shekh masoud Ali, Imamu wa Msikiti wa Maungani, alisema kwamba kimya cha Serikali tangu sheria kuanza kuvunjwa, kinawashawishi waamini kuwa jambo hilo linaungwa mkono na viongozi wa kitaifa.

“Rais wetu Dk Hussein Ali Mwinyi ni mtu mchamungu tunaamini atachukua hatua……licha ya kujenga wasiwasi kutokana na sheria kuanza kuvunjwa muda mrefu huku viongozi wa bodi wakiendelea kubaki katika vyazifa zao,” alisema Imamu Masoud.

Alisema viongozi wa bodi ya udhibiti wa vileo Zanzibar wanatakiwa kuchunguzwa na mamlaka za kusimamia sheria ili kufahamu kitendo walichokifanya, kimefanyika kwa maslahi ya umma au binafsi na kusababisha mtafaruku mkubwa katika jamii visiwani Zanzibar.

Alieleza kuwa lengo la kutungwa sheria mpya ilikuwa kudhibiti biashara ya vileo na kuondosha malalamiko ya kuongezeka baa katika makazi ya watu na karibu na huduma za jamii na kuleta kero kwa wananchi.

Kwa upande wake, Katibu wa bodi ya udhibiti wa vileo Zanzibar, Zainab Makame Sururu alisema mpaka Februari 22 mwaka huu, kampuni nane zilipewa vibali vya kuingiza vileo Zanzibar baada ya kila kampuni kulipa sh milioni 30 kabla ya kuruhusiwa kuingiza vileo Zanzibar.

Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Master Distiburors Limited, Sultan Cellers Limited, ZMMI Limited, One Stop Company Limited, QMB, Scotch Store, MGW (2014), Inteprises Company Limited na Ronak Store.

Hata hivyo Mwenyekiti wa bodi ya udhibiti wa vileo Zanzibar, Abdulrazak Abdulkadir, alisema kwamba sheria wameamua kuiweka kando ili kulinda mapato ya Serikali hasa kwa kuzingati Serikali ya awamu ya nane imekusudia kuimarisha ukusanyaji mapato.

“Tulitumia hekima na busara kulinda maslahi mapana ya mapato ya Serikali kwa kutoa vibali kwa kampuni za uagizaji pombe zaidi ya tatu,”alisema.

Kwa upande wake Mwanaharakati wa Haki za Binadamu Ali Makame Issa, alisema inasikitisha Serikali kushindwa kuvunja bodi mpaka sasa tangu ilipoanza kuvunja sheria ya udhibiti wa vileo Zanzibar na kusababisha malalamiko katika jamii na Jumuiya za dini Zanzibar.

Alisema Zanzibar ni nchi inayoendeshwa kwa kuzingatia misingi ya Katiba na Sheria lakini Serikali imeshindwa kuchukua hatua dhidi ya viongozi wa bodi ya vileo ambao wameamua kuvunja sheria kwa makusudi kuanzia Novemba mwaka jana.

“Kimya cha Serikali kinaonesha imeridhia sheria kuvunjwa wakati viongozi wameapa kulinda katiba na sheria ndio maana tumetaka serikali kuchukua hatua dhidi ya viongozi walioshiriki kuvunja sheria,”alisema Makame.

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar walipitisha sheria namba 9 mwaka 2020 na kuanza kutumika baada ya kusaidiwa na aliyekuwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Muhamed Shein Mei 11 mwaka jana na madhumuni ya kudhibiti biashara ya vileo Zanzibar na kuweka utaratibu mzuri wa uingizwaji wa vileo Zanzibar.

1 Comment

  • Hivisasa ni bora kuwe hakuna kuapa ili waendelee tu na unyama wanaotufanyia sababu hakuna maana yeyote kwa kiongozi kuchukua msaafuu na kuapa kwa kusema atasimamia katiba na sheria za zanzibar lakini akimaliza kuapaa anaanza kufanya anayoyajuwa yeye ambayo yapo nje ya kiapo na (katiba) huku kiongozi wa nchi pamoja na wasaidizi wake wakiyafumbia macho kana kwamba hawaoni. ujumbe umesha mfika rais Hussen Mwinyi akipuuzia zima yote ni kwake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

Habari za SiasaTangulizi

CAG aibua madudu halmashauri 10, TANESCO na MSD

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!