August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi yawagwaya “maninja” wa Lipumba

Lucas Mkondya, Kaimu Kamishna wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam

Spread the love

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema limekosa ushahidi kuhusu watu waliovamia mkutano wa Chama cha Wananchi – CUF, tarehe 22 Aprili, mwaka huu, anaandika Hamisi Mguta.

Lucas Mkondya, Kaimu Kamishna wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, amesema waliolalamika kuvamiwa katika tukio bado hawajapeleka ushahidi wowote hivyo bado jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wake na mpaka sasa halina ushahidi kamili wa kuwafikisha mahakamani watu hao.

Uvamizi huo ulifanywa na genge la watu wanaosadikika kuwa ni wafuasi wa Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa CUF anayetambulika na Msajili wa Vyama Vingi, ambapo watu hao waliwajeruhi waandishi na viongozi wa CUF huku mmoja wa wavamizi hao akinaswa.

Watu hao wakiwa wamejifunika nyuso zao, walivamia mkutano wa Juma Nkumbi, Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kinondoni katika hoteli ya Vina, Mabibo huku mmoja wa wavamizi hao akikamatwa na wananchi, na kisha kukabidhiwa kwa jeshi la polisi.

Hata hivyo polisi wanasema, “Polisi hatuwezi kufanikisha kesi ile (ya uvamizi), kama hatujapata ushahidi wa kutosha, tukio hilo bado tunaendelea na uchunguzi kwasababu kuna baadhi hawajajitokeza kutoa ushahidi kwahiyo niwatake waliovamiwa waje watoe ushahidi ili tuweze kwenda mahakamani,” amesema Kamanda Mkondya.

Kitendo cha polisi kutangaza kutokuwa na ushahidi wa uvamizi wa mkutano huo kimezuia hisia tofauti hasa kwa kuzingatia kuwa mmoja wa wavamizi alikamatwa lakini pia zipo picha za video zinazowaonesha wavamizi wakifanya tukio hilo.

Mbarala Maharagande, ameuambia mtandao wa MwanaHALISI Online, Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF Taifa amesema si kweli kwamba ushahidi juu ya wavamizi hao haukutolewa.

“Waliojeruhiwa wapo, mmiliki wa hoteli yupo pia na alikiri kutokea kwa tukio hilo, sasa sijaelewa kwanini jeshi la polisi linasema halijapata ushahidi, huku ni kutaka kukwepa tu majukumu yao,” amesema.

error: Content is protected !!