July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi yaanzisha timbwili Bonde la Mkwajuni

Spread the love

JESHI la Polisi leo lilivamia vibanda vilivyojengwa kwenye Bonde la Mkwajuni, Dar es Salaam na kuvichoma moto ili kuwaondoa wakazi waliokuwa wamevijenga baada ya nyumba zao kubomolewa mwishoni mwa mwaka jana. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Kabla ya polisi kuchoma vibanda hivyo, wananchi waliokuwa wakiishi kwenye bonde hilo waliifunga Barabara ya Kawawa kwenda Magomeni Moroko kwa zaidi ya saa moja pamoja na kuwasha moto na kusababisha foleni.

Uamuzi wa kufunga barabara hiyo ulifikiwa kutokana na wananchi hao kukasirishwa na hatua ya maofisa wa serikali kufika kwenye eneo hilo na kuweka alama ya X kwenye vibanda walivyovijenga baada ya nyumba zao kubomolewa kwenye eneo hilo.

Vurugu hizo zilianza baada ya zoezi lililokuwa likiendeshwa na Ofisa Mipango Miji, Dk. Charles Mkwarawa la kuweka alama za X kama ashirio la vibanda hivyo kubobolewa tena.

Katika zoezi hili vibanda zaidi ya 170 viliwekwa alama ya X ambapo Dk. Mkwarawa alidai kuwa, kuweka alama kwenye vibanda hivyo ni agizo la serikali na wizara husika.

Mkuregenzi wa Baraza la Mazingira (NEMC), Bonventure Baya amesema kuwa serikali ilitoa taarifa muda mrefu na tayari wameanza baadhi ya hatua hivyo zoezi la kuweka alama kwenye vibanda si la kushtukiza na kwamba, zoezi hilo litaendelea na serikali imeamua kusafisha maeneo yote yaliyobomolewa.

“Endapo wananchi watakaidi kuondoka kwenye maeneo hayo serikali itachukua hatua kama ilivyofanya leo na kwamba hakuitajiki kuwepo kwa uchafu wowote kwenye maeneo haya,” amesema Baya.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa, moto huo ulichomwa baada ya ofisa mipango miji kufika na askari kweye eneo hilo na kuweka alama ya bomoa ambapo wananchi waliamua kwenda kuchoma matairi ya gari barabarani na kusababisha moto mkubwa kuwaka na hivyo kusababbisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Hatua ya wananchi hao kuchoma moto barabarani iliwasukuma polisi kuchukua hatua ya kuchoma vibanda vyao ambavyo tayari vilikuwa vimewekwa alama ya X. Kwa mujibu wa wananchi hao tayari vibanda saba vilikuwa vimechomwa moto bila ya wamiliki wake kuwepo.

Wananchi hao wameeleza masikitiko yao kuwa, Rais John Magufuli ameanza kuwatia machungu wananchi mapema huku wakidai kwamba hawataondoka kwenye maeneo hayo.

“Hapa hatutoki hata kama wametuchomea vibanda vyetu kwa sababu sisi hatukupewa viwanja hata nyumba zetu hazikuwekwa alama ya X na kwamba tayari wameshatuchomea magodoro yetu na mali zetu hivyo hatutoki tunataka watuue,” alizungumza mmoja wa wananchi hao.

Stumai Issa ni mkazi wa jirani wa Bonde la Mkwajuni ambapo amesema kuwa, kitendo cha wananchi kuchoma moto barabarani kinaonesha ni jinsi gani wananchi walivyochoka kunyanyasika nchini mwao na wanataka rais apate ujembe huu. “Kufunga barabara ni ujembe tosha kwa rais.”

Athumani Kishitu ni miongoni mwa watu waliounguziwa moto vibanda vyao na polisi kutokana na tukio la kuwasha moto barabarani ambapo amesema, alikuwa amejipumzisha kibandani kwake ghafla akawaona askari na maofisa wengine wakizunguka kibanda hicho na kuamuriwa kuwa ahame baada ya siku tatu huku wakimuwekea alama ya X.

Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mwajuma aliyekuwa analia kutokana na kuchomewa moto kibanda chake amesema kuwa, serikali imekosa huruma kiasi cha kuchoma moto vibanda vyao walivyokuwa wanajisitiri.

“Serikali inataka tukakae wapi ilhali nyumba zetu wametuvunjia na leo tena wametuchomea moto vibanda vyetu, najisikia uchungu sana maana kwenye kibanda changu askari bila kujua, walitaka kumchoma moto mtoto wangu aliyekuwa amelala ndani,” amesema.

Hata hivyo, vurugu hizi zimesababisha wananchi watano kukamatwa kwa tuhuma za kuhusika.

error: Content is protected !!