September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi wazuia mkutano wa Mbowe Morogoro

Spread the love

JESHI la Polisi Wilaya ya Morogoro limezuia mkutano wa hadhara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) uliotarajiwa kufanyika kesho Jumapili tarehe 16 Juni 2019, kwa kile ilichoeleza kwamba ni kutokana na sababu za kiusalama. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Mkutano huo ulipangwa kufanyika hapo kesho katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege, ambapo Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, alitarajiwa kuhutubia kwenye mkutano huo kama mgeni wa heshima.

Taarifa ya zuio hilo imetolewa leo tarehe 15 Juni 2019 na Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) katika ukurasa wake wa Twitter, huku ikiambatanisha barua ya Jeshi la Polisi wilayani Morogoro kuhusu kusitisha mkutano huo.

“Jeshi la Polisi wilaya ya Morogoro limesitisha mkutano wa hadhara wa Chadema uliokuwa unatarajiwa kufanyika siku ya kesho Jumapili, Juni 16, 2019. Jeshi la Polisi limesitisha mkutano huo kwa kile walichokieleza kuwa ni sababu za kiusalama,” inaeleza taarifa ya BAVICHA.

Barua ya polisi imeeleza kuwa, chama hicho hakijapewa kibali cha kufanya mkutano wa hadhara na shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege.

“Nakujulisha kwamba, hamtaruhusiwa kufanya mkutano huo wa hadhara kwa sababu za kiusalama. Ni matumaini yetu kwamba mtashirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutii sheria mkizingatia kaulimbiu yetu ya Utii wa Sheria bila Shuruti,” inaeleza sehemu ya barua hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro, SP. J.J Kahambwa.

error: Content is protected !!