WATU watatu wanaozaniwa majambazi wameuawa katika majibizano ya risasi na Polisi wilayani Nyamagana mkoani Mwanza wakati walipokaidi amri ya Polisi ya kujisalimisha eneo la tukio, anaandika Moses Mseti.
Miezi sita iliyopita Jiji la Mwanza liligubikwa na vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha za moto na kusababisha zaidi ya watu 10 kupoteza maisha huku majambazi wanne kuuawa na Polisi katika kipindi hicho.
Katika mauaji hayo yaliyotokea usiku wa jana saa mbili na nusu usiku pia jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata silaha mbili bastora aina ya Duty CZ 75P -07 yenye namba B.512637 ikiwa na risasi 15 na magazini mbili.
Aina nyingine ya silaha iliyokamatwa katika mpambano huo kati ya Polisi na majambazi hao ni Short Gun iliyofutika namba ikiwa na risasi mbili na maganda mawili ya risasi.
Majambazi hao waliouawa wamefahamika kwa majina ya Benedidicto Thobias, Mabula Segeja na Charles Thomas waliojeruhiwa kwa risasi na baadae kufariki dunia wakati wakipelekwa hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC).
Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akidai kwamba awali walifanikiwa kumkamata mganga wa kienyeji, Ayub Nyamweru mkazi wa Katoro mkoani Geita aliyetoa taarifa hizo.
Msangi amesema kuwa mtuhumiwa huyo alipohojiwa na askari aliwataja wenzake wanafanya nao uhalifu wakiwamo majambazi watatu waliouawa na Polisi katika majibizano hayo ya risasi.
“Baada ya kupata taarifa hizo Polisi walienda kuweka mtego eneo la tukio (viwanja vya St. Marys) ndofye Kata ya Igoma, walipokuwa wamepanga kukutana kwa ajili ya kupanga mipango ya kwenda kufanya uhalifu,” amesema Msangi.
Hata hivyo Msangi amesema kuwa usiku huo huo wa saa 2:30 wenzake watano na mtuhumiwa huyo (Mganga) walifika eneo la tukio ndipo askari walipowaamuru kujisalimisha na kukaidi amri hiyo na kuanza kufyatua risasi na askari wakajibu.
Msangi amesema kuwa Bastora hiyo iliyokamatwa ilikuwa ni mali ya Suleiman Waziri mkazi wa Nyamongolo ambayo alikuwa anaimiliki kihalali na short gun iliyofutika namba.
Miili ya majambazi hao, imehifadhiwa katika Hospitali ya rufaa ya Bugando kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi huku msako wa kuwasaka wenzao ambao wametoroka na wengine waliyokuwa wanashirikiqna nao.
Hata hivyo, upelelezi wa wali unadai kwamba majambazi hao na wenzao wamekuwa wakifanya matukio ya uvunjaji wa nyumba usiku na kufanya unyang’anyi na kubaka pindi wanapovunja nyumba za watu usiku.
Kamanda Msangi, anatoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Mwanza kuendelea kutoa taarifa sahihi na za mapema za uhalifu kwani wanawahafamu.
Leave a comment