July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi watuhumiwa kwa mauaji Tunduma

ACP Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza

Spread the love

JESHI la Polisi mkoani Mbeya, limetuhumiwa kumuua kijana Sajo Sanga (27) kwa kumpiga na kitako cha bunduki wakati wa wakizima vurugu katika Mji mdogo wa Tunduma wilayani Momba. Anaandika Mwandishi wetu … (endelea).

Sanga anadaiwa kufariki tarehe 21Machi mwaka huu, saa tano usiku wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Kanda iliyopo jijini Mbeya.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Mpoki Ulisubisya amesema Sanga alifikishwa hapo tarehe 19 Machi mwaka huu, saa tano usiku kutoka Tunduma na kugundulika akiwa na majeraha sehemu kubwa ya tumboni.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, Sanga alipigwa na kitako cha bunduki eneo la tumbo na mmoja ya askari waliokuwa wakituliza vurugu hizo.

Wakati sakata hilo likiendelea, pia mwananchi mwingine, Adelina Mlowe bado anaendelea na matibabu kutokana na mimba yake ya miezi nane kuharibika na kuondolewa kizazi wakati akikimbia bomu lililopigwa na polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) katika vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahamed Msangi amesema jeshi hilo halina taarifa za kifo wala mtu kujeuriwa katika vurugu hizo.

Licha ya kamanda kukana, lakini Adelina amehamishiwa katika hospitali ya Rufaa Mbeya kitengo cha Wazazi- Meta na pia, Diwani wa Kata ya Tunduma, Frank Mwakajoka ni mmoja wa watu walioumizwa na polisi kwa kuvunjwa mkono wake wa kushoto, huku watu zaidi ya 100 wakishikiliwa.

Kamanda Msangi amesema katika vurugu hizo zilizodumu kwa siku tatu, watu 26 wamepandishwa kizimambani akiwemo Mwakajoka na kwamba bado jeshi linawashirikilia baadhi ya watu.

Diwani Mwakajoka ameiomba Tume ya Haki za Binadamu kufika Tunduma na kuona vitendo vya kinyama vilivyofanywa na polisi.

error: Content is protected !!