JESHI la polisi Mkoa wa Dodoma limetoa ufafanuzi juu ya kifo cha Ustadhi Rashid Ally Musa maarufu kwa jina la Rashid Ramadhani Bura (62). Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).
Jeshi la polisi limetoa ufafanuzi kutokana na kutokea kwa utata na kauli mbalimbali ambazo zimeonekana kuichanganya jamii na wakazi wa Mkoa wa Dodoma kwa ujumla.
Kamada wa polisi Mkoa wa Dodoma ASCP Gilles Muroto, alisema kuwa jeshi la polisi lilibaini kuwa kifo cha Bura kilitokana na ugonjwa wa moyo.
Muroto alisema kuwa marehemu Bura ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya The Dalai Islamic Centre na Mmiliki wa shule ya Zamzam ambaye makazi yake yalikuwa Chang’ombe Extension jijini Dodoma alipatwa na mauti akiwa ofisini kwake kutokana na shinikizo la moyo.
Kamanda Muroto alisema kuwa kabla ya kifo chake tarehe 21 Desemba, 2019, alihudhuria Mkutano wa Mahusiano ya dini mbalimbali huko Jijini Dar es Salaam na kurejea Dodoma siku iliyofuata kwa kutumia usafiri wa basi namba T980 DNN la kampuni ya Kimbinyiko .
Alisema kuwa marehemu alikata tiketi namba 1947 na alipata siti namba 13 na baada ya kufika Dodoma alifikia ofisini kwake mtaa wa Barabara ya Nyerere, Kata ya Madukani Jijini Dodoma, na akiwa ofisini kwake alipatwa na tatizo la moyo na alizidiwa na kufariki dunia kwa kukosa msaada wa karibu.
“Kutokana na safari yake hiyo, alikosa mawasiliano na ndugu zake baada ya simu yake kuzima, na kwa kuwa ndugu walifahamu kuwa amesafiri, waliendelea kumtafuta kwa njia ya simu bila mafanikio, pia waliwasiliana na watu wengine aliokuwa nao katika safari hiyo hawakufanikiwa.
“Ilipofika tarehe 25 Desemba, mwaka huu, majira ya saa 11:00 jioni mtoto ake Ally Mussa alikwenda ofisini kwake na kukuta amefariki duniani na mwili wake ukiwa umevimba, unatoa harufu na umeharibika kutokana na kukaa takribani siku nne.
“Jeshi la polisi lilifika eneo la tukio na wataalam wa uchunguzi wa matukio kuchunguza tukio hilo, eneo la tukio ulifanyika uchunguzi na upekuzi katika ofisi yake na kugundua kuwa hakukuwa na uharibifu wowote katika ofisi yake, hakuna wizi wowote wa mali, upekuzi ulifanyika na lilikutwa begi dogo la nguo chacheza safari, simu yake ikiwa imezima, tiketi ya safari, Pesa katika pochi Sh. 260,000 na vitambulisho vyake.
“Mwili wa marehemu ulipelekwa hospitali ya Rufaa ya Dodoma na kufanyiwa uchunguzi na daktari kuthibitisha kuwa, kifo chake ni moyo kufeli na kushindwa kufanya kazi, hata hivyo jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea kufanya uchunguzi kupitia simu zake kubaini kama kuna taarifa za ziada, na watu wasitumie taarifa ya kifo hiki kupotosha umma au kuunda taarifa zenye upotoshaji kama zinavyoenezwa mitandaoni,” alieleza Muroto.
Leave a comment