May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi watatu wasota kwa utakatishaji fedha

Spread the love

MAOFISA watatu wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha na wafanyabiashara watano, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya mkoani humo kwa makosa sita ikiwemo utakatishaji fedha Sh. 10 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Polisi hao Heavenlight Mushi mwenye namba G. 5134 DC, aliyekuwa polisi kitengo cha Intelijensia Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, jijini Dar es Salaam; Bryton Murumbe, mwenye namba za kiaskari H.1021 PC na Gasper Paul, mwenye namba H.125 PC aliyekuwa akifanya kazi kwenye kitengo cha Intelijensia Makao Makuu Dodoma.

Watuhumiwa wengine ni Lucas Mdeme, mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, jijini Arusha; Nelson Lyimo, mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite; Joseph Chacha maarufu ‘Baba Ngodo,’ na Leonila Joseph Omary Alphonce (43) maarufu kwa jina la Matelephone.

Watuhumiwa hao wamepandishwa kizimbani na kushitakiwa kwa makosa sita yakiwemo uhujumu uchumi, utakatishaji fedha.

Jana tarehe 13 Januari 2020, Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Adelaide Kassalay na Agnes Hyera mbele ya Rose Ngoka, Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Arusha, walidai kuwa shitaka la kwanza linawakabili mshitakiwa wa kwanza, pili na watatu  ambao ni polisi.

Kwamba, tarehe 5 Desemba  2020, walijihushisha na uhalifu huku wakitambua kuwa, wao ni watumishi wa umma na kujipatia rushwa kiwango cha awali  kiasi cha Sh. 10 milioni kutoka kwa Sammy Mollel, mkurugenzi wa Kampuni ya Gems & Rock Venture ya jijini Arusha.

Kassalay alisoma shitaka la pili linalowakabili washitakiwa wanne ambao ni Baba Ngodo, mshtakiwa wa tano joseph, mshtakiwa wa sita Lyimo, mshtakiwa wa saba Mdeme na mshtakiwa wa nane Matelephone, wote wanashitakiwa kwa kujifanya watumishi wa umma na kuunda mtandao wa kihalifu na kupanga njama za kujipatia fedha taslimu Sh. 10 milioni kutoka kwa Mollel.

Kassalay alisoma, shitaka la tatu linalowakabili watuhumiwa wote nane ambalo ni la kupanga njama za kuhujumu uchumi ikiwa tarehe 5 Desemba 2020, walijipatia fedha Sh. 10 milioni kutoka kwa Mollel.

Kassalay alidai kuwa, shitaka la nne linamkabili Chacha mshitakiwa wa nne ambaye anatuhumiwa akiwa na nia kufanya uhalifu, udanganyifu na kujitambulisha kuwa yeye ni mtumishi wa umma Ikulu.

Kassalay alidai, shitaka la tano linalowahusisha washitakiwa wote kwa kufanya udanganyifu na kujipatia fedha kiasi cha Sh. 10 milioni za awali kati ya Sh. 10 milioni ili wamwachie huru kwa tuhuma za kukwepa kodi na kufanya biashara ya madini ya Tanzanite kwa kutorosha madini nje kinyume cha sheria.

Kassalya alisoma shitaka la sita la utakatishaji fedha haramu linalowakabili washitakiwa wote, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa wote kwa pamoja tarehe 5 Desemba 2021, walipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Sh. 10 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Sammy Mollel.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo ,Hakimu Ngoka alisema watuhumiwa hawatakiwi kujibu chochote juu ya mashtaka yao kwa kuwa mahakama hiyo, haina uwezo wa kisheria kusikiliza shauri hilo.

Shauri hilo limeahirishwa mpaka tarehe 27 Januari 2021, kwa ajili ya kutajwa, watuhumiwa wamerejeshwa rumande.

error: Content is protected !!