January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi watajwa kuua

Spread the love

JESHI la Polisi mkoani Pwani limeingia katika tuhuma za mauaji ya kijana aliyefikishwa kituoni Mkuranga, akidaiwa kupora pochi yenye simu. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Masoud Saidi Hamadi wa umri wa miaka 28, aliripotiwa kufa Jumamosi ya Septemba 5, mwaka huu saa kadhaa baada ya kufikishwa kituo kikuu cha Mkuranga.

Awali mtuhumiwa alipelekwa kituo cha polisi Vikindu, baada ya kukamatwa akiwa mgahawa wa mama yake mdogo hapo Vikindu.

Dada wa marehemu, Ganji Abdallah amesema ndugu yake alikamatwa akiwa mzima wa afya, na hakuleta fujo yoyote.

“Walikuja kumkamata wakiwa na Afisa Mtendaji, askari polisi wawili wa kituo cha Vikindu,” amesema. Aliwataja askari hao kwa jina mojamoja – Zungu na Innocent.

Mlalamikaji aliyeripoti kuporwa pochi na mtuhumiwa ametambuliwa kuwa ni Glory Mbuzi ambaye pia anaishi Vikindu.

Mjomba wa marehemu, Said Masoud amezungumza na Mwanahalisi Online, akisema alipata taarifa kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) majira ya saa 7 mchana Jumamosi kutoka kwa Afisa wa Polisi kwamba mpwawe amefikishwa kituoni.

“Baadaye nilikwenda kituo cha Vikindu, lakini niliambiwa amepelekwa kituo cha Mkuranga,” amesema mjomba huyo.

Mama mdogo wa marehemu, Fatma Masoudi amesema ameshangazwa kupata taarifa ya msiba wa mtoto ambaye aliambiwa yupo mikononi mwa polisi.

“Nilipigiwa simu na mtoto wa kaka anaitwa Mahafudhi na kunipa taarifa hizo ndipo tukaongozana mpaka kituo cha polisi cha Mkuranga ambako Mkuu wa Polisi Wilaya Mkuranga alitueleza kuwa hana taarifa zozote,” amesema.

Amesema msaidizi wa mkuu wa kituo ndiye aliyewapa taarifa ya uthibitisho wa kifo cha Masoudi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jaffari Mohammed alipoulizwa kuhusu tukio hilo, amesema Masoudi alifariki dunia kutokana na afya yake kutokuwa nzuri.

“Afya yake ilikuwa si nzuri na kifo ni mipango ya Mungu,” amesema lakini alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa mtuhumiwa aliuawa, alisema, “Mtu yeyote hata kama ni askari polisi akikutwa na makosa atawajibishwa.”

Hata hivyo, Iddi Hassani ambaye aliuona mwili wa marehemu Hospitali ya Taifa Muhimbili jana, amesema mapema kuliibuka utata kuhusu hatua ya madaktari wa Hospitali ya Wilaya Mkuranga kugoma kuchunguza mwili wa marehemu kwa kudai hawakuwa na vifaa.

“Tuliuona mwili wa marehemu ukiwa na majeraha kwenye baadhi ya sehemu na nywele zake zilinyonyoka, uso ukiwa na majeraha na miguuni kukionekana vijidonda na damu,” alisema Hassani.

Ndugu wa marehemu walikubali kuchukua mwili leo na ilitarajiwa kwenda kuuzika Temeke, Dar es Salaam.

error: Content is protected !!