August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi waondoa zuio la mikutano ya vyama

Spread the love

JESHI la Polisi hapa nchini, limetengua marufuku ya mikutano ya ndani ya vyama vya siasa ambayo liliitatangazwa mwezi mmoja uliopita, anaandika Pendo Omary.

Tarehe 24 Agosti, mwaka huu jeshi hilo, lilipiga marufuku mikutano yote ya vyama vya siasa, ikiwemo vikao vya ndani kwa madai kuwa mikutano hiyo ilikuwa ikichochea uvunjifu wa amani, hata hivyo leo limesema limejiridhisha kuwa, hali ya kiusalama ni ya kuridhisha.

Marufuku hiyo ilitangazwa katika wakati ambao Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilikuwa katika maandalizi ya uzinduzi wa operesheni ya ‘Umoja wa Kupinga Udikiteta Tanzania’ (Ukuta), kikilenga kuzindua mikutano na maandamno nchi nzima kuanzia Septemba mosi mwaka huu.

Akizungumza na Waandishi wa leo jijini Dar es Salaam, Nsato Marijani, Kamishna wa Opereshani na Mafunzo wa Jeshi la Polisi amesema, wamefuatilia mwenendo wa shughuli za vyama vya siasa na kubaini kuwa, kwa sasa hali ipo shwari.

“Jeshi la Polisi limekuwa likifuatilia hali ya usalama hasa inayohusiana na shughuli za vyama vya siasa na sasa limejiridhisha kwamba kumekuwepo na hali ya kuridhisha kiusalama na hivyo kuona hakuna hoja ya kiusalama kuendelea kuzuia mikutano ya ndani ya vyama,” Amesema.

Hata hivyo Jeshi la Polisi limeendelea kushikilia msimamo wake wa kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya kisiasa ambao pia ulitolewa na Rais John Magufuli.

“Kuanzia leo tarehe 22 Septemba, 2016 tunaondoa katazo la mikutano ya ndani ya vyama siasa, lakini maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ispokuwa ile ya wabunge katika majimbo yao bado imezuiliwa hadi tahimini pana zaidi ya hali ya usalama itakapofanyika,” amesema Marijani.

 

error: Content is protected !!