September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi wamuonya Prof. Lipumba, Maalim Seif

Spread the love

JESHI la Polisi Zanzibar limesema, litashughulika kikamilifu na mfuasi yeyote wa Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), ama Maalim Seif Sharif Hamad (ACT-Wazalendo) iwapo watatibua amani iliyopo sasa visiwani Zanzibar. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Kumekuwepo na kauli za vitisho kwa maofisa wa CUF dhidi ya ACT-Wazalendo visiwani Zanzibar, kwamba wanajiandaa kupoka ofisi zinazotumiwa na chama hicho (ACT-Wazalendo) kwa madai, ni mali yao (CUF).

Jeshi hilo limewataka viongozi hao wawili, na vyama vyao kumaliza migogoro yao kwa amani, na kwamba hawatokuwa tayari kuona wanatowesha amani iliyopo sasa visiwani humo.

Akizungumza na MwanaHALISI ONLINE kwa simu leo tarehe 7 Desemba 2019, Suleiman Hassan Suleiman, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, amesema vyombo vya ulinzi havitavumilia uvunjifu wa sheria.

Kamanda Suleiman amewataka wafuasi wa Maalim Seif, Mshauri Mkuu wa ACT-Wazalendo na Prof. Ibrahim Lipumba, kuhakikisha wanatuliza mihemuko ya wafuasi wa vyama vyao huku wakisubiria uamuzi wa mahakama kuhusu mgogoro huo, badala ya kutumia nguvu katika kuusuluhisha.

“…wajielekeze kufuata sheria sababu mali ya mtu haiwaniwi kwa nguvu. Hatuwezi kuwania mali kwa nguvu, kama kuna tatizo zaidi warudi mahakamani.

“Mahakama ikiwapa kibali baada ya kuthibitisha kama mali zao, wakachukue (CUF). Kama watatumia nguvu, vyombo vya ulinzi na usalama havitavumilia uhalifu. Vitachukua hatua,”ameonya Kamanda Suleiman.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Hassan Nassir Ali, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kaskazini Pemba amevishauri vyama hivyo kusubiri maamuzi ya kesi ya msingi Na. 16/2019 iliyofunguliwa na CUF kwenye Mahakama Kuu ya Vuga, kuhusu mgogoro huo.

“Ninafahamu wamepeleka kesi mahakamani, na kama waungwana inabidi wafuate utaratibu wande mahakamani.  Wanapoanza kubishana katika vyombo vya habari wakati kesi yao iko mhakamani, sio uungwana,” amesema SACP Ally na kuongeza;

“Wasubiri maamuzi, mahakama ikiamua nani mwenye mali, sisi polisi tunafuatilia kuhakikisha mwenye mali anapata haki yake. Kwa hiyo hilo suala wafuate taratibu. Kwa ufupi, hatuhusiki na mgogoro wa watu wanaogombea mali lakini wakipigana, tutaingia kulinda usalama.”

Tarehe 4 Desemba 2019, Mussa Haji Kombo, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini CUF alitangaza kwamba, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho limeeleza mali zake zinazodaiwa kuporwa na ACT-Wazalendo, zirejeshwe.

Kombo alieleza zaidi kuwa, CUF iko katika utaratibu wa kurejesha mali hizo, ikiwemo ofisi na samani za ofisi. Miongoni mwa ofisi za CUF zinazodaiwa kuporwa na ACT-Wazalendo ziko visiwani Pemba na Unguja, Zanzibar.

Tamko hilo, lilijibiwa na ACT-Wazalendo kupitia Joran Bashange, Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi ya chama hicho, akisema kwamba hawatishiwi na tamko hilo, na kuwa wanawasubiri CUF waje kuchukua kama hizo mali ni zao.

Khalifa Suleiman, Katibu Mkuu wa CUF amesema, CUF lazima itazirejesha mali zake, na hakuna wa kuwazuia.

“Kwa kuwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF-Chama Cha Wananchi limeazimia kurejesha ofisi zake zilizoporwa na ACT,  kupitia kikao chake cha Tarehe 12 na 15, 2019, sisi viongozi tuzirejesha ofisi zetu asubuhi kweupe,” amesema Suleiman.

Suleiman amemtaka Maalim Seif na wafuasi wake, kuwepo wakati CUF inachukua mali zake

“kama wewe hodari wa kutuzuia sisi tusijekuchukua mali zetu, tunakuomba na wewe uwepo kama ulivyowaagiza wafuasi wako na viongozi wenzio wa ACT muwepo , ” amesema Suleiman.

Hivi karibuni, Maalim Seif ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa CUF, na baadaye kutimkia ACT-Wazalendo kutokana na mgogoro wake na Prof. Lipumba, alidai CUF kwa kushirikiana na CCM, wamepanga kufanya vurugu kwa lengo la kukamata viongozi wa chama chao na kuwaweka ndani.

 

error: Content is protected !!