September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Polisi ‘wamtii Lissu’, Serikali yafanya hiyana

Spread the love

TAMKO la Tundu Antipas Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akilitaka Jeshi la Polisi kuacha kuwashikilia watu 10 waliokamatwa kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo uchochezi, limeanza kutekelezwa kwa shingo upande, anaandika Faki Sosi.

Jumamosi iliyopita, Lissu alilitaka jeshi hilo kuacha kuvunja Katiba na Sheria za nchi kwa kuwashikilia watuhumiwa hao zaidi ya wiki mbili badala ya kuwafikisha mahakamani ndani ya masaa 48, kama sheria zinavyoelekeza.

“Tunalitaka Jeshi la Polisi kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani siku ya Jumanne ya wiki ijayo la sivyo tutalifikisha jeshi hilo mahakamani ili likajieleza kwa uvunjifu wa Sheria na Katiba,” alisema Lissu katika tamko lake jumamosi ya wiki iliyopita.

Baada ya tamko hilo la Lissu, Jeshi la Polisi lilianza kuwasafirisha watuhumiwa liliowakamata mikoa mbalimbali na kuwaleta Dar es Salaam.

Siku ya juzi jeshi hilo liliwasafirisha watuhumiwa Ignasia Mzenga wa Morogoro na Alex John wa Dodoma ili kuwarudisha katika mikoa waliyokamatiwa huku Mdude Nyagali na wenzake watatu wakisafirishwa kwenda Mkoa wa Songwe siku ya jana.

Jijini Dar es Salaam polisi imewafikisha mahakamani mahabusu watano miongoni mwa kumi iliokuwa ikiwashikilia, hata hivyo waendesha mashitaka wa serikali hawakuandaa hati ya mashitaka ya watu hao na hivyo kusababisha kutopandishwa kizimbani.

Kufuatia kitendo hicho, Lissu ameiambia MwanaHALISI Online kuwa waendesha mashtaka wa serikali wamefanya roho mbaya na uzembe wa makusudi kutoandaa mashitaka ya watu hao licha ya kuwashikilia kwa muda wa siku 20.

“Haiwezekani kukaa na watuhumiwa kwa siku 20 halafu leo wanakuja mahakamani bila ya kuwa na hati ya mashtaka, ina maana walikuwa hawajui wanataka kuwafungulia kesi gani? Huu ni uzembe mkubwa kwa serikali hii na waendesha mashitaka wake,” amesema Lissu.

Lissu ameeleza zaidi akisema, “tulitegemea watu hawa wapandishwe kizimbani leo lakini hali imekuwa tofauti, serikali imeshindwa kuandaa hati ya mashitaka kwa makusudi na kwa kweli dhamira yetu ya kufungua kesi ya kulishtaki Jeshi la Polisi na serikali ipo pale pale.”

…………………………………………………………………………………………………..

Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia (bonyeza)> Simgazeti kwa wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel. Pia unaweza kupakua (download) app ya Mpaper au Simgazeti kutoka kwenye playstore.

error: Content is protected !!