July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Polisi wamduwaza Sumaye

Spread the love

FREDERICK Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ameshangazwa na unyongaji demokrasia unaofanywa kwa kiwango kikubwa nchini, anaandika Dany Tibason.

Ametoa kauli hiyo jana mjini Dodoma muda mfupi baada ya Jeshi la Polisi kutumia nguvu kutawanya wanafunzi na wanachama wa Chadema Vyuo Vikuu Mkoa wa Dodoma (CHASO) wakati wakifaya mahafali yao ya saba kwa ajili ya kuagana.

Amesema, kitendo cha serikali kulifanya taifa lisiwe na nafasi ya kukosolewa ni dalili mbaya ya udikiteta na kamwe haiwezi kufumbiwa macho.

Amesema, hakuna serikali yoyote duniani ambayo inaweza kukataa kusemwa kwani kiongozi bora na shupavu ni ule ambaye anasemwa na kusikiliza watu wanasema nini.

Sumaye ambaye alikuwa awe mgeni rasmi katika mahafari hayo ambapo amesikitishwa na kitendo cha polisi kuzuia mahafali ya wanafunzi hao kwa kuwa ni haki yao kuagana na kubadilishana uongozi.

Amesema, imekuwa ni aibu kwa serikali kuendesha nchi kwa matakwa ya mtu mmoja jambo ambalo amesema ni kujenga chuki kwa wananchi hata pale ambapo hapakuwepo na sababu.

Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Zanzibar amesema, bado uongozi wa Chaso unafanya tathimini ya kuona ni jinsi gani ya kufanya taratibu juu ya Jeshi la Polisi kuwasababishia hasara wanafunzi hao.

Amesema, pamoja na jeshi hilo kuingilia mahafali hayo, bado wanafanya maandalizi ya kuhakikisha mahafari hayo yanafanyika ili vijana hao waweze kupata haki yao.

Mwalimu amesema, kwa sasa serikali inaogopa upinzani na kamwe nguvu ya upinzani haitaweza kupunguzwa hata kwa siku moja na badala yake inazidi kuimarika.

Lazaro Mambo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma amesema, sababu za kuzuia mahakafali hayo ni kutokana na kuwepo kwa taarifa za uvunjifu wa amani.

Hata hivyo amesema, licha ya kuwepo kwa taarifa hizo tayari Jordan Lugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alikuwa ametoa zuio la kuwepo kwa mikutano ya kisiasa katika mkoa huo.

error: Content is protected !!