April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Polisi wajichanganya, Bil 1.2 zawatokea puani

SACP Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Jeshi la Polsii Kanda Maalumu ya Dar es Salaam

Spread the love

ASKARI Polisi tisa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kosa la kukiuka maadili ya kazi wakati wa ufuatiliaji wa sakata la wizi wa Sh. 1.2 bilioni uliofanywa na wafanyakazi wanne wa Kampuni ya Ulinzi ya G4S. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam…(endelea).

Pia, kanda hiyo inawashikilia wafanyakazi hao wa Kampuni ya G4S kwa tuhuma za wizi wa Sh. 1.2 bilioni, Dola za Marekani 402,000 na Euro 27,700, mali ya Benki ya NBC.

Taarifa hiyo imetolewa leo tarehe 25 Februari 2020 na SACP Lazaro Mambosasa, Kamanda wa Jeshi la Polsii Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wakati akizungumza na wanahabari.

Kamanda Mambosasa amewataja watuhumiwa hao kuwa ni, Christopher Rugemalila (34) ambaye alikuwa dereva wa G4S, mkazi wa Chanika, Mohamedi Ramadhani( 40) mkazi wa Mtoni Kijichi, Salimu Shamte (45) mkazi wa Mbagala Kizuiani, Ibrahimu Maunga (49), Mkazi wa Kiluvya.

Kamanda Mambosasa amedai kuwa, watuhumiwa hao walitekeleza uhalifu huo tarehe 7 Februari 2020, baada ya kutokomea kusikojulikana na fedha hizo ambazo walielekezwa kuzipeleka makao makuu ya Benki ya NC yaliyoko Posta ya zamani.

Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo, Kamanda Mambosasa amesema watuhumiwa hao walitelekeza gari ya kampuni ya 4GS iliyokuwa imebeba fedha hizo, baada ya kuzihamishia katika gari binafsi iliyokuwa inaendeshwa na Salumu Shamte.

“Walinzi hao walikabidhiwa fedha kutoka tawi la benki ya NBC Kariakoo na Samora ili wazipeleke makao makuu, lakini hawakufanya hivyo, matokeo yake walipanga njama na kuelekea maeneo ya Temeke Maduka Mawili karibu na kituo cha mafuta cha Camel,” amesema Kamanda Mambosasa.

Kamanda Mambosasa amesema baada ya uhalifu huo kutokea, Jeshi la Polisi liliunda kikosi kazi kilichofuatilia watuhumiwa hao na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa wa kwanza ambaye ni Regemalila, aliyekamatwa tarehe 17 Februari 2020 maeneo ya Mongo la Ndege.

“Rugemalila alikamatwa na alipopekuliwa alikutwa na Tsh. 110,000,000, Dola 19,000 zikiwa ndani ya gari lake na magari matano. Baada ya kuhojiwa alikiri kuchukua fedha hizo na kusema kwamba amenunua nyumba mbili na kiwanja kimoja vyenye thamani ya 107,000,000,” amesema Kamanda Mambosasa na kuongeza.

“Tarehe 21 watuhumiwa wawili walikamatwa (Mohamedi na Salimu) maeneo ya Mbagala, na walipopekuliwa walikutwa na Tsh. 332,000,000, Dola za Mareknani 50,000, Euro 5010 na gari iliyotumika kubebea fedha.”

error: Content is protected !!