Friday , 1 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Polisi waendeleza Sinema kuhusu Lissu
Habari za SiasaTangulizi

Polisi waendeleza Sinema kuhusu Lissu

Sheikh Ponda, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislam Tanzania (kushoto)
Spread the love

SASA inavyoonesha ni kama vile Jeshi la Polisi Tanzania (TPF) linafikiri watu kuzungumzia chochote kuhusu Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ni haramu kisheria. Wamo katika harakati za kuhangaikia wanaotoa maoni kuhusiana na maendeleo ya mbunge huyo na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Kwa siku kadhaa sasa, Jeshi la Polisi linafuatilia maelezo ya watu mbalimbali na hasa viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yanayosambazwa kupitia vikao na waandishi wa habari pamoja na ndani ya mitandao ya kijamii.

Hatua hii imethibitika kwa namna Inspekta Jenerali wa Polisi Simon Sirro anavyosikika akisema katika ziara yake ya nchi nzima kutembelea askari na vikosi vya jeshi hilo. Sirro ametoa kauli zinazoelekea kujibu yale yaliyotamkwa na viongozi wa Chadema, chama ambacho Lissu pia ni kiongozi wake mwandamizi.

Katika siku za karibuni, IGP Sirro amesikika akisema uchunguzi wa jaribio la kumuua Lissu kwa risasi, unazorota kwa sababu dereva wake, Simon Michael, yuko nje ya nchi. Kwamba anatakiwa kuhojiwa kwa anachokijua juu ya tukio hilo la Lissu kushambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari ambayo dereva huyo alikuwa anaendesha wakitokea bungeni mjini Dodoma.

Na katika kauli nzito, akasema ni marufuku kwa watu kuzungumzia taarifa za Lissu kwa kuwa tukio lililompata uchunguzi wake unaendelea.

Lissu yuko hospitalini jijini Nairobi, Kenya, anakotibiwa majeraha mengi aliyoyapata sehemu mbalimbali za mwili baada ya kufyatuliwa risasi zaidi ya 30 alipokuwa anawasili nyumbani kwake eneo la Area D, mjini Dodoma.

Shambulio hilo lilifanywa mchana kweupe tarehe 7 Septemba 2017, na watu waliokuwa wamebeba bunduki wakiwa kwenye gari ambalo dereva wa Lissu alieleza kupata kuliona kabla likiwa na watu wanaoonesha kuwafuatilia wao tangu maeneo ya bunge mjini Dodoma.

Pamekuwa na hali ya mvutano kati ya viongozi wa Chadema na Serikali kuhusu matibabu yake na uchunguzi wa shambulio dhidi ya Lissu hasa kwa kuwa uongozi wa juu wa chama hicho ndio umekuwa msimamizi wa matibabu ya Lissu wakiwa karibu na familia yake – mkewe na ndugu zake.

Serikali ilijitoa kumtibu Lissu pale familia yake iliposhikilia kuruhusiwa kumchukua ili kumtibu nje ya nchi. Uamuzi wa serikali kutoshughulikia matibabu ya Lissu ulitamkwa katika kikao cha mashauriano kati ya Chadema na Serikali, ikiwakilishwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Spika wa Bunge, John Ndugai. Hoja ilikuwa kwamba serikali ingegharimia matibabu hayo yakifanywa chini ya uratibu wa madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Watu mbalimbali wanakwenda Nairobi kumkagua Lissu. Lakini hakuna kiongozi hata mmoja wa serikali aliyeripotiwa kufika kwa ajili hiyo. Baada ya kuonekana Lazaro Nyalandu, mbunge wa Singida Kaskazini, ambaye anatokea Chama Cha Mapinduzi (CCM), wiki iliyopita alionekana Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF).

Jana mchana, Sheikh Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, alitoa taarifa kuwa amemuona Lissu na kuzungumza naye machache. Akasema ameumia. Ndipo akasema anataka kukutana na waandishi wa habari Jumatano ili kueleza umma kuhusu safari yake hiyo, iliyoanzia na shughuli za kijamii nchini Kenya.

Hapana shaka tamko lake lilivuta “macho, masikio na hisia” za uongozi wa Jeshi la Polisi. Walijiandaa kukabiliana naye uso kwa uso. Kwa bahati nzuri au mbaya, Sheikh Ponda akawa jasiri kuliko. Alifanya mkutano wake mpaka mwisho. Akaondoka haraka baada ya kujibu maswali machache ya waandishi.

Sekunde chache baadaye, kama vile alijua akizubaa atanasa katika mtego wa dola, wakatokea askari wa Polisi. Hawakumkuta na wakajikuta wanaangushia waandishi wa habari lile pupa waliloenda nalo kwenye eneo ambako Sheikh Ponda alifanyia mkutano wake.

Askari waliobeba silaha waliwasili saa 5 hivi, saa nzima kabla ya muda ambao Sheikh Ponda aliahidi kufanya mkutano wake.

Waliwasiliana na uongozi wa hoteli na kushuhudiwa wakipekua chumba baada ya chumba hotelini kujiridhisha kama Sheikh Ponda hakujificha. Hawakumuona. Mmoja wa waandishi wa habari aliyekuwepo, Karoli Vicent aliiambia MwanaHALISI Online kuwa askari hao walifika na kuamuru waandishi wasiondoke mpaka wampate Sheikh Ponda.

Walipomkosa, mwandishi anasema, polisi walimchukua mwandishi wa Z4 News, Ahmed Kombo, na kwenda naye kituo cha polisi ili awasaidie kupata picha za video alizopiga wakati Sheikh Ponda akizungumza na waandishi.

Haikufahamika haraka kama Polisi wanaendelea kumtafuta Sheikh Ponda ambaye katika mkutano wake na waandishi wa habari, alisema kuna umuhimu mkubwa kwa mamlaka ya serikali kufanya uchunguzi kuhusu ukatili aliofanyiwa Lissu. Pia akazungumzia kufanywa uchunguzi wa miili kadhaa ya watu iliyookotwa maeneo ya ufukwe wa Coco Beach, jijini Dar es Salaam.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mgomo kitita kipya cha NHIF: Serikali yaita hopsitali binafsi mezani

Spread the loveSERIKALI imekiita mezani Chama cha Wenye Hospitali Binafsi (APHFTA), ili...

Habari za Siasa

Wapinzani wamlilia Rais Mwinyi

Spread the loveVYAMA vya siasa nchini Tanzania, vimetuma salamu za rambirambi kufuatia...

Habari za Siasa

Wananchi Dar watakiwa kujitokeza barabarani kumuaga Hayati Mwinyi

Spread the loveWANANCHI wasiokuwa na muda wa kwenda katika Uwanja wa Uhuru,...

Habari za SiasaTangulizi

Mwili wa Hayati Mwinyi kuagwa leo saa 8 Uwanja wa Uhuru

Spread the loveMWILI wa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi unatarajiwa kuagwa kuanza...

error: Content is protected !!