January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi wadaiwa kutishia kuua waangalizi

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Njombe Fulgence Ngonyani

Spread the love

BAADHI ya askari Polisi mkoani Njombe wanadaiwa kuwavamia, kuwateka, kuwashambulia na kutishia kuwaua waangalizi wa uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia mfumo wa kielektoniki (BVR). Anaandika Pendo Omary… (endelea).

Walioshambuliwa ni Humphrey Josian na Wilson Raphael- waangalizi kutoka Mtandao wa Asasi za Kiraia wa Kuangalia Uchaguzi Tanzania (TACCEO), unaoratibiwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC

Kwa mujibu wa TACCEO, tukio hilo limetokea tarehe 7 Machi mwaka huu, majira ya saa 4.45 usiku, chumba namba tano kwenye nyumba ya wageni ya Neto iliyopo Makambako mjini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Martina Kabisana- Mwenyekiti wa TACCEO amesema, utekaji na utesaji huo ulifanywa na askari polisi sita.

“Waliwaweka chini ya ulinzi mhudumu na mlinzi wa nyumba hiyo. Mlinzi akafungiwa chooni. Askari wawili walibaki kuwalinda mlinzi na mhudumu.

“Askari wanne wakiwa na silaha mbili za moto- bunduki aina ya SMG, waliwavamia Josiah na Raphael na kuwashambulia kwa kuwapiga mateke na marungu huku wakiwataka waoneshwe kompyuta walizoiba Mufindi,” amesema.

Kabisama ameongeza kuwa askari hao walitekeleza ukatili huo wakiwa wamevalia kiraia na hawakujitambulisha kama taratibu zinavyoelekeza.

“Kibaya zaidi, muda wote walitoa vitisho vya kuwaua waangalizi wetu kwani walikuwa wamewaelekezea bunduki na kuwatishia,” amefafanua Kabisama.

Baada ya kutekeleza unyama huo na kugundua kuwa waangalizi hao sio wahalifu, inadaiwa kuwa askari hao waliomba radhi na kuondoka bila msaada hasa kwa Raphael aliyeumia miguu baada ya kupigwa na virungu na vitako vya bunduki.

“Baada ya tukio hilo, waangalizi wetu walijikusanya na kumsaidia Humphrey ambapo walienda naye polisi na kupewa PF-3 na kupatiwa matibabu. Hali ya Humphrey bado hairidhishi,” ameongeza

Kufutia tukio hilo, TACCEO imelitaka jeshi la polisi kuwataja hadharani askari walioshiriki katika tukio hilo na kueleza hatua zilizochukuliwa dhidi yao.

Pia imeitaka serikali kuwahakikishia wadau wote wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi usalama wao kipindi chote cha uandikishaji wapiga kura, kura ya maoni na uchaguzi mkuu.

“TACCEO tutaitisha mkutano mkubwa wa wadau wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi ili kujadili tishio la usalama tunapokuwa katika shughuli za uchaguzi,” amesema Kabisama.

Adha ameongeza kuwa TACCEO itawapa msaada wa kisheria Josia na Raphael ili kufungua kesi ya kikatiba ya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na askari

error: Content is protected !!