January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi waanza kuibeba CCM

Spread the love

JESHI la Polisi jijini hapa, limeanza kutumika kwa kukibeba Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya askari Polisi, kugeuka wanaccm kwa kuwasimamia wafuasi wa CCM kuchana bendera za Chadema. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Tukio hilo limetoa leo mjini hapa baada ya wafuasi wa CCM kuanza vurugu za kuchana bendera za Chadema huku askari wa kutuliza ghasia (FFU) wakiwa wamewasimamia na kuwafukuza wale wa Chadema.

Hali hiyo ya Polisi kuanza kutumika na CCM imeelezwa kuwa chanzo cha machafuko katika uchaguzi mkuu utakaofanyika nchi nzima kesho.

Hata hivyo Polisi hao ambao walishuhudiwa na mwandishi wa habari hizi, wakiwa wanaburuzwa na wafuasi wa CCM ambao walikuwa wakipeleka wanavyotaka wakati wakichana bendera hizo.

Katika kile kilichoonekana wafuasi wa Chadema kutokukubaliana na mchezo wa Polisi kuwabeba CCM pia na wao walianza kuondoa bendera za CCM na kusababisha mvutano mkali.

Polisi baada ya kuona hali hiyo inakuwa ngumu iliwalazimu kufuata matakwa ya wafuasi wa Chadema, ambao walikuwa wakipita wakiimba huku wakitaja jina la Mgombea Urais wa chama hicho, Edward Lowassa kwamba ndio chaguo lao huku Polisi wakiwa nyuma.

Mmoja wa Wafuasi wa Chadema, Jumanne Dau, amesema kitendo hicho cha Polisi kuibeba CCM na kushindwa kutenda haki, kutasababisha machufuko kipindi hiki cha uchaguzi.

“Tanzania hakuna haki na hakuna amani bali tuna uvumilivu na uvumilivu huu, utakuwa mwisho kesho, Polisi wanageuka wanaccm,” amesema Dau huku akitokwa na machozi.

Tukio hilo la wafuasi wa CCM kuchana bendera za Chadema, linadaiwa kuanza usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi, pia linadaiwa kuratibiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo.

Hata hivyo Mulongo ambaye anadaiwa kuapa kwamba Jimbo la Nyamagana ni lazima lirudi katika himaya ya chama chake, limeonekana kuota mbawa kutokana na wananchi wengi kuunga mkono muungano wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, alikiri kuwepo kwa baadhi ya Polisi kuibeba CCM na kwamba baada ya kupata taarifa hizo waliweza kulitatua.

“Suala la Polisi kuagizwa kuibeba CCM, halipo na hakuna agizo kama hilo, ndo maana baada ya kupata taarifa nimeingilia na sasa hali ipo swali,” amesema Mkumbo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, kupitia simu yake mkono haikuweza kupokelewa.

error: Content is protected !!