MSEMAJI wa Jeshi la polisi Tanzania David Misime SACP amewataka waandishi wandishi wa habari kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kukuza maslahi mapana ya Taifa pale wanapokuwa wakifanya kazi zao au wanapokuwa katika midahalo mbalimbali. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma (endelea).
Misime ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Septemba 2023 alipokuwa akifungua mdahalo wa kitaifa kuhusu ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari ulioandaliwa na Umoja wa vyama vya waandishi nchini (UTPC).
Mdahalo huo ulikuwa na kauli mbiu isemayo, “Shambulio la lolote kwa mwandishi wa habari ni shambulio kwa umma”.
Akifungua mdahalo huo kiongozi huyo wa polisi amesema kazi kubwa ya jeshi la polisi ni kulinda raia na mali zake lakini pia kuhakikisha usalama wa polisi, waandishi pamoja na jamii kwa ujumla.
“Waandishi mnatakiwa kuandika habari ambazo zitakuwa na uwezo wa kulifanya taifa kuwa na sifa ya kuwavutia wawekezaji kuingia nchini bila kuwa na shaka yoyote jambo ambalo litafanya nchi kuwa katika utulivu,” amesema Misime.
Pamoja na mambo mengine Misime amesema waandishi wakishirikiana vyema na jeshi la polisi hata kwa kufichua au kutoa taarifa sahihi ni wazi watakuwa salama na polisi atakuwa salama sambamba na wananchi kwa ujumla wake.
Naye Mkurugenzi wa UTPC, Kenneth Sembaya ambaye amesema kuwa ni wajibu wa mwandishi wa habari kufanya kazi yake kwenye mazingira rafiki bila kubughudhiwa.
Sembaya amesema iwapo mwandishi wa habari atakuwa anafanya kazi kwa kunyimwa uhuru hali hiyo itasababisha watanzania kukosa habari na mwandishi wa habari mwenyewe kushindwa kutimiza wajibu wake.
Aidha, amesema mwandishi wa habari anatakiwa kufanya kazi kwa kupewa uhuru na kulindwa anapokuwa katika mazingira rafiki kwa lengo la kutimiza majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya taifa.
Leave a comment