October 23, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Polisi wa Mafia tuhumani

Spread the love

POLISI Wilaya ya Mafia inatuhumiwa kumpiga na kumtesa kijana mwendesha pikipiki (bodaboda) na kumnyima fomu ya kupatia matibabu (PF3) hospitalini na hivyo kuendelea kuishi na maumivu. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Mohammedi Fakihi, anayeishi mtaa wa Kigamboni eneo la Kilindoni, Mafia, ameiambia MwanaHALISI Online kwa njia ya simu kuwa anaendelea kuugulia maumivu kwa siku ya nne kwa sababu ya kukosa matibabu.

Analalamika kujisikia maumivu maeneo ya kiuno, mgongo, mikono na miguu, baada ya kile alichoeleza “kupigwa kipigo cha mbwa mwizi akiwa nje ya kituo na kwenye kituo cha polisi cha Mafia,” amesema.

Akieleza tukio lilivyotokea, Fakih amesmea Jumatatu majira ya saa 10 alasiri akiwa anatoka msibani kwa kipikipiki aliyompakiza mama yake, alitokea mtu asiyemjua na ambaye alikuwa amevaa nguo za kiraia.

Alisimamishwa na mtu huyo na kutakiwa amkabidhi ufunguo wa pikipiki yake, lakini alikataa na kumuomba ajitambulishe kwanza kwa vile hakuwa anamfahamu.

Alieleza kuwa jibu la kutakiwa kujitambulisha, lilikuwa ni kwa mtu huyo kumsukuma na kumtoa kwenye pikipiki na kuanza kumpiga ngumi za mfululizo.

Fakih amesema hakumpa ufunguo mtu huyo kutokana na kuwa hakumtambua ni nani kutokana na hofu ya kuibiwa pikipiki alimtaka mtu huyo amuoneshe kitambulisho cha kuthibitisha kuwa yeye ni Ofisa wa Jeshi la Polisi.

“Nilipomtaka kitambulisho alichukia na kunishusha kwa nguvu kwenye pikipiki, akaninyang’anya ufunguo na kuanza kunipiga ngumu mfululizo huku mama na dada wakishuhudia,” amedai.

Baadaye, mtu huyo alimuita mwenzake waliokuwa pamoja na kumchukua Fakih mpaka kituo kikuu cha Polisi cha Mafia ambako ndiko alikopata jina la aliyemmpiga akiitwa kwa jina la Magai.

“Nilijua kuwa aliyenikamata na kunishambulia ni askari baada ya kufika kituoni ambako alishirikiana na wenzao wanne na kuendelea kunipiga kwa kuchangiana kama vile wamemkamata mtuhumiwa wa mauaji,” amedai Fakih.

“Nasikitika kuwa askari wanampiga virungu na mateke raia kama mbwa mwizi bila ya kumueleza kosa lake… mpaka wananiachia nikiwa niliyeishiwa nguvu, sikuelezwa kosa langu ni nini.

Analalamika kuwa alilazimishwa kunywa hadi kuyamaliza maji yaliyokuwa kwenye ndoo kituoni huku akiwa anapigishwa mchura mpaka akashindwa kusimama mwenyewe.

Mjomba wa Fakih ambaye alipata taarifa za tukio hilo, alifika kwenye kituo hicho kwa ajili ya kumwekea dhamana na kupata nafasi ya kumsaidia kupata matibabu.

Hata hivyo, hakupatiwa fomu ya matibabu na kulazimika kumchukua bila ya fomu hiyo.

“Hivi tunavyoongea Fakih anaendelea kulalamika maumivu maeneo mbalimbali ya mwili lakini hatuna vya kumsaidia kutokana na kutoipata PF3… ni ukatili mkubwa unaofanywa na Polisi dhidi ya raia,” amesema.

Mwandishi wa habari hizi aliwasiliana na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), aliyetambuliwa kwa jina moja la Max, ambaye hata hivyo hakutoa ushirikiano.

“Mimi si msemaji wa Jeshi la Polisi, mpigie RPC,” alisema na kukataa katakata hata kama anajua kuwepo kwa tukio hilo.

Inajulikana Mafia ni moja ya wilaya mbalimbali nchini ambazo wakuu wake (OCDs) wameruhusiwa kutoa taarifa za matukio kutokana na kuwa maeneo ya mbali na makao makuu ya polisi mkoa.

MwanaHALISI Online iliwahi kuchapisha taarifa za tukio kama hilo Septemba mwaka huu, lakini ambalo mtuhumiwa alifariki mikononi mwa polisi kwenye kituo cha Polisi Mkuranga, mkoani Pwani.

Aliyepigwa hadi kufa kituoni alikuwa Masoud Said Ahmadi ambaye alikamatwa nyumbani kwao na kufikishwa kituoni ambako siku ya pili ndugu zake walipomfuatilia, waliambiwa ndugu yao amefariki.

Polisi walidai kuwa alikuwa anaumwa tangu alipokamatwa, madai yaliyopingwa na ndugu wa marehemu.

error: Content is protected !!