July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi Tanzania, mmewaona wenzenu wa Guinea ya Ikweta

Askari wa Malabo, Guinea ya Ikweta wakiwakinga wachezaji wa Ghana ili wasipigwe na mashabiki wa Guinea ya Ikweta baada ya mchezo kumalizika

Spread the love

VURUGU zilizotokea katika mchezo wa nusu fainali ya pili ya Fainali za Mataifa Afrika kati ya wenyeji Guinea ya Ikweta na Ghana, zimetia dosari fainali hizo, lakini ni funzo wa askari wa Tanzania. Anaandika Erasto Stanslaus.

Mchezo huo ulilazimika kusimama kwa zaidi ya nusu saa baada ya mashabiki wa Guinea ya Ikweta kuanza kurusha chupa uwanjani na kuwashambulia mashabiki wa Ghana ambao walilazimika kukimbilia uwanjani ili kunusuru maisha yao.

Polisi wa jijini Malabo walifanya kazi ya ziada kuwatuliza mashabiki hao kwa kutumia helkopta na walipofanikiwa mchezo huo uliendelea kwa dakika tatu za nyongeza.

Katika harakati za polisi kuwatuliza mashabiki hao hakukuwa na tukio la kutumia nguvu wala kupigwa mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya, bali busara ilitumia kwa kiasi kikubwa.

Polisi walilazimika kuwashawishi wachezaji wa timu ya Guinea ya Ikweta kwenda kuwaomba mashabiki wao watulie ili wamalizie mchezo huo, hali iliyosaidia kushushwa jazba na wapenzi hao wa soka ambao hawakukubaliana na kilichotokea uwanjani.

Tukio zima la mchezo huo ni funzo kwa askari wetu ambao wanakuwa uwanjani na wale ambao wanakuwa katika matukio kama hayo nje ya uwanja.

Misimu mitatu iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara, polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi katika mchezo kati ya Simba na Kagera Sugar ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, kisa mashabiki waling’oa viti na kuvitupia uwanjani baada ya wapinzani wao kupewa penalti dakika za mwisho.

Ukifananisha tukio la Simba dhidi ya Kagera na lile ya jana huko Malabo, tukio lilotokea katika nusu fainali hiyo lilikuwa kubwa, lakini haikutumika nguvu kubwa kuimaliza, tofauti na lile la mashabiki wa Simba.

Kama tukio la Malabo lingetokea nchini bila shaka mchezo ule usingeendelea, kwani yangefyatuliwa mabomu ambayo hayachagui mchezaji, shabiki, wala mwamuzi wote wangetawanyika na ndiyo ungekuwa mwisho wa mchezo.

Mabao ya Ghana katika mchezo huo yalifungwa na Jordan Ayew kwa penalti dakika ya 42, Mubarak Wakaso dakika ya 45+1 na Andre Ayew dakika ya 75.

Ghana sasa itamenyana na Ivory Coast katika fainali ya AFCON 2015 Jumapili, wakati hatma ya wenyeji na mchezo wa mshindi wa tatu dhidi ya DRC haijajulikana, kwani kuna uwezekano wakapewa adhabu kali na CAF.

error: Content is protected !!