September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Polisi ruksa kuua

Spread the love

 

JESHI la Polisi limeamriwa kuua mtu yeyote ataedaiwa kuwa jambazi, anaandika Moses Mseti.

Ruhusa hiyo imetolewa leo na Ahmed Msangi, kamanda mpya wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP).

Msangi ambaye amehamia mkoani humo akitokea Mbeya, ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na maofisa usalama na polisi wa vyeo mbalimbali baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi hiyo na SACP, Justus Kamugisha.

Msangi ametoa kauli hio siku chache baada ya John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kusema kwamba, Kamugisha alikuwa mzigo kwenye jiji hilo kutokana na kushindwa kukabiliana na ujambazi.

Katika kipindi cha miezi miwili ya Machi na Aprili mwaka huu, matukio saba ya uhalifu wa kutumia silaha za moto umeripotiwa na katika matukio hayo watu sita walipoteza maisha.

Msangi amesema kuwa, anawashangaa polisi wanaoshindwa kutumia silaha zao kuwaua watu wanaodaiwa kuwa majambazi na kusababisha vitendo vya uhalifu kuendelea kushamiri jijini humo.

“Tumieni na nyie bunduki zenu kuua watu ambao ni majambazi, haiwezekana uwe na silaha halafu unaacha kuchukua hatua za haraka za watu ambao wanasababisha mauaji na uporaji wa mara za raia,” amesema Msangi.

Msangi amesema, Jiji la Mwanza miezi michache iliyopita limetikiswa na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha yanayoambatana na mauaji ya raia, kujeruhi na uporaji wa mali zao.

Amesema kuwa, polisi wanapaswa kufanya kazi zao kwa kujiamini na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Kamanda Kamugisha akikabidhi ofisi hiyo aliwahimiza polisi kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya jeshi hilo bila kumuonea mtu yeyote yule.

 

error: Content is protected !!