August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Magufuli achonganisha Polisi, Mgambo Mwanza

Askari wakilanda katika mitaa ya jiji la Mwanza baada ya kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga)

Spread the love

AGIZO la Rais John Magufuli kutaka wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama machinga kurejeshwa katikati ya jiji la Mwanza limezua jambo kufuatia mgambo wa jiji hilo kuingia katika mvutano mkali kiasi cha ‘kushikana mashati’ na askari polisi, anaandika Moses Mseti.

Hatua hiyo inatokana na mgambo wa jiji la Mwanza kuendelea kushikilia mizigo ya wafanyabiashara hao wakidai malipo (posho) baada ya kufanya kazi ya kuwaondoa machinga katikati ya jiji hilo kwa siku nne.

Baada ya taarifa za kusitishwa kwa zoezi hilo, mgambo hao walikusanyika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambako walianza kufanya fujo wakishinikiza kulipwa posho zao.

Mgambo hao walieleza kuwa wanahitaji kulipwa posho zao kwa kazi waliyofanya baada ya zoezi la kuwaondoa machinga kusitishwa huku wakiwa hawajalipwa stahiki zao.

“Tupo jumla ya mgambo 500 na tulikubalina kuwa tutalipwa posho Sh. 30,000/= kwa siku, hata hivyo kwa siku tatu za zoezi hilo tumelipwa Sh. 45,000/= tu.

Ndiyo maana unaona watu tuna wasiwasi kwasababu tunafahamu kazi zikiisha kama hivi zoezi lilivyosimamishwa itakuwa ngumu kulipwa haki yetu,” amesema mgambo huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake.

Katika hatua nyingine, askari Polisi mmoja ambaye jina lake halikufahamika, amejikuta akiangushiwa kipigo na mgambo hao wakati akiwatetea machinga waliokuwa wakichukua bidhaa zao zilizokuwa zikishikiliwa.

Tukio hilo limetokea katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, ambapo polisi walikuwa wakiwazuia mgambo wasiwapige watu walioenda kuchukua bidhaa zao katika ofisi hiyo.

Marry Tesha, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi ili kuzungumzia suala la mgambo hao kufanya fujo wakishinikiza kulipwa posho zao, simu yake ilikuwa ikiita na kukatwa.

error: Content is protected !!