August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi Manyara wahakikisha ulinzi siku za Sikukuu

Karatu mjini

Spread the love

JESHI la Polisi mkoani Manyara kupitia msemaji wake, Kamanda wa Jeshi hilo mkoani hapa, Francis Jacob Masawe, amewahakikishia wakazi wa mkoa huo ulinzi na usalama wakati wa kusheherekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya, anaandika John Walter.

Kamanda Masawe ametoa tahadhari za kiusalama kuhusiana na sikukuu hizo katika wakati akizungumza na MwanaHALISI Online akieleza kuwa yeyote atakayebainika kuleta uvunjifu wa amani jeshi halitamvumilia.

Ameongeza kuwa mpaka sasa vikosi katika kila wilaya na mijini vimeshapangwa kwa ajili ya kufanya doria za kiusalama na kuahidi kuchukua hatua za kisheria kwa wale watakaosheherekea sikukuu hizo kwa namna inayokiuka sheria na kuhatarisha usalama.

Aidha Kamanda Masawe amesema baadhi ya wahalifu hutumia vipindi vya sikukuu kufanya vitendo vya kihalifu, lakini akaonya kuwa yeyote atakayejaribu kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali kwa sababu wamejipanga kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaendelea kudumishwa wakati wote.

Kesho kutwa, Watanzania wataungana na watu wengine duniani kote kusherehekea Krismasi kabla ya kufuatiwa na siku ya kupeana zawadi (Boxing Day) katika siku inayofuata na Jumapili ya wiki ijayo itakuwa ni Mwaka Mpya.

“Tumejipanga vya kutosha, siwezi kuweka mbinu hadharani hapa kwa sababu za kiusalama, lakini itoshe tu kuwaambia kwamba Jeshi la Polisi liko vizuri na asithubutu mtu yeyote kufanya uhalifu mahali popote maana tuna mkono mrefu tutamkamata,” amesema Masawe.

Kwa upande mwingine amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kufikisha taarifa haraka wanapobaini kuwa kuna mtu, kundi au watu wanaowatilia shaka, huku kila mmoja akiwa mlinzi wa jirani yake katika biashara, makazi na mahali pengine.

“Ukiona kuna mtu anaingia kwa jirani yako halafu humfahamu au unamtilia shaka, mpigie simu au piga simu polisi kupitia namba 111 na 112,” amesema.

Ameongeza kuwa jeshi hilo limejipanga pia kwa kuimarisha ulinzi katika maeneo ya kuabudia, sehemu za starehe na maeneo mengine ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.

Masawe aliwataka waendeshaji wa kumbi za starehe kuzingatia uhalali wa matumizi ya kumbi zao na kuepuka kuzidisha idadi ya watu tofauti na uwezo wa kumbi zao na kwamba kwa yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali.

error: Content is protected !!