January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi “wamkumbatia” Chenge

Andrew Chenge

Spread the love

JESHI la Polisi mkoani Simiyu, limemkingia kifua Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge (CCM), kwamba bastola yake sio iliyotumika kufyatua risasi hewani kuwatisha wafuasi wa Chadema kama inavyodaiwa. Anaandika Yusuf Katimba… (endelea).

Badala yake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi, anasema “katika msafara ule kulikuwa na mtu anaitwa Ahmed Ismail aliyekuwa na bastola. Alipiga risasi tatu juu ili kuwatawanya watu wakaweza kuondoka.

Utetezi wa kamanda unakizana na ule wa wafuasi wa Chadema, wanaodai kuwa Chenge-aliye pia Mwanasheria Mkuu mstaafu wa Serikali, aliwafuata katika ofisi zao mjini Bariadi na muda mfupi baada ya kushuka kwenye gari, alifyatua risasi hewani.

Madai ya Chadema yametolewa na Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha), John Heche ambaye awali ndiye alihutubia wafuasi hao akiwa na Katibu wa baraza hilo taifa, Julius Mwita.

Chenge hakupokea simu yake kujibu madai hayo, lakini Heche ameliambia MwanaHALISIOnline kuwa “baada ya kumaliza mkutano, wafuasi wa Chadema walitusindikiza kuelekea katika ofisi za chama kusaini kitabu cha wageni.”

Heche ameongeza kuwa, wakiwa ofisini, Chenge alifika eneo hilo na msafara wa wafuasi wa CCM wakiwa ndani ya magari kama sita ambayo yalikuwa yakipiga nyimbo za kuisifu CCM, jambo lililowakera wafuasi wa Chadema waliokuwa nje.

“Tulipoona sintofahamu imeanza kutokea kwa wafuasi wa pande zote mbili, nikatoka nje na kumwona Change anashuka katika moja ya gari. Niliamua kumfuata ili kumtaka aondoke eneo hilo kwa walikuwa wamevamia msafara wetu bila sababu ya msingi,”anasema.

Heche anaongeza kuwa, “wakati namfuata Chenge kabla hata sijamfikia, alitoa bastola na kufyatua risasi tatu juu, na hapo ndipo vurugu zilipoanza.”.

Anasema kuwa hatua hiyo ilisababisha taharuki kubwa ya watu kukimbia hovyo, na hivyo yeye pamoja na viongozi wenzake kulazimika kutoa taarifa kituo cha polisi na kupewa Kumb namba BAR/RB/1195/2015.

Anafafanua kuwa “jambo la ajabu, tulipofika kituoni, Chenge tayari naye alikuwa amefika, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa dhidi yake.

Maelezo ya pande zote yanaibua maswali kadhaa. Kwa mfano; ni wafuasi wa chama kipi waliwafuata wenzao. Kwanini walifanya hivyo. Polisi waliotoa vibali vya mikutano walikuwa wapi. Mfyatua risasi alitumia taratibu gani. Heche anamfahamu Chenge au. Tumwamini Heche aliyeshuhudia tukio au kamanda aliyepewa taarifa?

MwanaHALISIOnline, halikupata majibu ya kutosheleza kutoka kwa Kamanda Mushi. Badala yake amesema, “kulikuwa na mikutano miwili; wa Chadema uliofanyika kwenye uwanja wa Basketball na ule wa CCM uliofanyika Isanga Kilometa 10 kutoka mjini.

Anasema kuwa baada ya mikutano wafuasi wa vyama hivyo walitawanyika, na kwamba CCM walipokuwa wakirudi mjini kupitia barabara kuu huku gari la Chenge lilikuwa likipiga mziki tangu walipoondoka mkutanoni.

“Walipofika eneo linaloitwa Mwisho wa Lami karibu na ofisi za Chadema, Chenge alishuka kuwasalimia watu ambao walikuwa wakicheza mziki akidhani ni wafuasi wa CCM, na aliposhuka ndipo aliposikia amri ya ‘piga mawe’ na hivyo akarudi kwenye gari lake,” amesema Mushi.

Alipoulizwa uzito wa tukio na matumizi ya silaha za moto kama vinaendana, “amesema haoni tatizo kwa kuwa risasi hazikumlenga mtu.Risasi ya moto inakuwa na matumizi mabaya pale inapomlenga mtu. Sijaona hoja ya msingi hapo. Silaha ndogo ni ya mtu kujilinda mahali popote.”

Amesema kuwa, silaha hiyo inamilikiwa na Ismail kihalali na kwamba wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo

error: Content is protected !!