KAMISHNA wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, CP Nsato Marijani amesema Jeshi la Polisi linakwenda kufanya operation kali dhidi ya majambazi waliohusika na mauaji ya askari nane wilayani Kibiti, Pwani, anaandika Hamisi Mguta.
CP Marijani ameyasema hayo ikiwa ni masaa kadhaa yamepita baada ya kundi la watu waliosadikika kuwa ni majambazi kushambulia askari na kuwauwa kisha kuwapora silaha.
“Kama nilivyosema tunakwenda kwenye operation yamoto, hili tukio halina ukubwa zaidi ni kwamba tumepoteza askari wetu lakini wale ni majambazi tu si lolote si chochote, tutawashuhulikia na hakuna atakayebaki,” amesema.
Amesema kuwa kwakua matukio ya mauaji yametokea hata kwa wenyeviti wa mitaa ambapo wenyeviti wasiozidi 32 wamewahi kuuawa hivyo tukio hilo si la kufanyiwa mzaha.
“Tunakumbuka matukio ya nyuma ya uvamizi wa vituo vya polisi na ni zaidi ya mara kumi hili sasa halivumiliki,” amesema.
Askari ambao wameripotiwa kuuawa na kundi hilo la majambazi ambalo idadi yake haijafahamika ni A/INSP Peter Kigugu, F.3451 CPL Francis, F.6990 Pc Hauna, G.3247 pc Jackson, H.1872 Pc Zacharia, H.5503 Siwale, H.7629 PC Maswi na H.7680 PC Ayoub.
Kundi hilo liliwashambulia askari hao waliokua katika gari la Polisi PT. 3713 Toyota L/Cruiser na kumjeruhi askari mmoja no F.6456 PC Fredrick kwa kumpiga risasi ya mkono wa kushoto na amepelekwa katika Hospitali ya Misheni Mchukwi kwa matibabu.
CP Marijani amesema suala la kujenga kambi katika maeneo yaliyo na misitu inayoonekana kuwa machimbo ya watu wabaya kama majambazi, haliwezi kufanyika katika maeneo yote nchini kwa sababu nchi inamapori mengi na kusisitiza kuwa tukio hilo linatekelezwa na kikundi kidogo cha watu ambao polisi wanauwezo wa kuwadhibiti.
“Hiki ni kikundi kidogo na wala hawana ujasili wowote, tuseme ukweli wanapora, wakiua wanachukua siraha kwa hiyo ni majambazi, waporaji, wanaoijua jografia ya eneo la Mkuranga, Rufiji, Kibiti, Ikwiriri, ni sehemu zenye watu wachache, ndiyo maana wanajibana katika misitu kutokana na eneo lilivyokubwa,” amesema.
Ameeleza kuwa matukio ya mauaji yanatokea sana kwa polisi kwa sababu ndiyo wanaowazuia watu hao wabaya kufanya mambo yao hivyo kujenga vita dhidi ya polisi ambao wanalinda usalama ili wasitekeleze mambo yao.
“Jeshi lenye dhamana ya kulinda raia na watu zao ni polisi ndiyo maana mapambano yatakayoonekana yataonekana kati ya jeshi la polisi na majambazi hao kwa sababu wanaopambana nao ni jeshi la polisi ambao wanawazuia kutekeleza vitendo vyao ni jeshi la polisi,” amesema.
Hata hivyo amesisitiza kuwa: “Hilo si tukio la kigaidi, nchi hii haina ugaidi watu wasingeweza kutembea kwa amani, hiki ni kikundi tu cha majambazi na watapatikana hivi karibuni.”
Kwa upande mwingine CP Marijani amesema eneo ambalo tukio la mauaji limetokea ni marufuku kuendesha pikipiki kuanzia 12 jioni, hakuna pikipiki zitakazoruhusiwa kutembea.
Leave a comment