August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polisi kuchunguza utata vifo vya mapacha Dar

Spread the love

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limeanza uchunguzi wa vifo vya vijana mapacha waliofahamika kwa jina la Khalifu na Khalifa, ambao wanadaiwa kupoteza maisha baada kunyweshwa dawa kwenye dua waliyokwenda kusomewa ili kutibu matatizo ya kukabwa na watu wasiojulikana usiku. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI Online, kwa njia ya simu, leo Jumamosi, tarehe 23 Julai 2022, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Jumanne Muliro amekiri kutokea kwa tukio hilo.

Amesema taarifa hizo wamezipata na wanazifanyia uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha vifo vya vijana hao.

“Sisi hizo taarifa tulizipata, kama kawaida kazi yetu tunachunguza hizo taarifa,” amesema Kamanda Muliro.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika familia ya mapacha hao, Khalifu na Khalifa walifikwa na umauti Jumamosi iliyopita, baada ya kupewa dawa inayodaiwa kuwa ni sumu na mama anayedaiwa kuwafanyia dua, maeneo Buza Mnarani, wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.

Ally, ambaye ni Kaka wa Khalifu na Khalifa, akizungumza na wanahabari hivi karibuni kuhusu tukio hilo, alidai kabla ya mapacha hao hawajafariki dunia, walimpigia simu kumuomba awafuate kwa mama aliyekuwa anawafanyia dua.

Baada ya kufika alimkuta Dotto akiwa amepoteza fahamu huku Kulwa akiwa anatapatapa, ambapo waliwapeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, ambapo madaktari waliwaeleza kuwa Dotto amepoteza maisha, baada ya muda hali ya afya ya Kulwa ilibadilika na kisha kupoteza maisha.

Ally alidai kuwa, enzi za uhai wao, mapacha hao walikuwa wanasumbuliwa na tatizo la kukabwa na watu wasioonekana muda wa usiku, huku akidai hata yeye amekumbana na tatizo hilo mara kadhaa na kwamba huwa anafanyiwa dua.

Mama wa mapacha hao, naye alidai watoto wake walikuwa na tatizo la kukabwa na watu wasiojulikana usiku.

Kwa mujibu wa kaka wa marehemu, mapacha hao walizikwa kijijini kwao Msanga, na kwamba mama anayedaiwa kuwapa dawa hiyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.

error: Content is protected !!