April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Polisi Hai ‘wamkaba’ Mbowe

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Spread the love

MIKUTANO ya hadhara yenye lengo la kufanya mrejesho kwa wananchi kuhusu kazi zilizofanywa na mbunge wao, Freeman Mbowe, katika jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro, imezuiwa na Jeshi la Polisi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Barua iliyoandikwa na Jeshi la Polisi kwa Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, imedai sababu za kuzuia mikutano yake ni za kiusalama.

Hata hivyo, barua hiyo imeeleza, Lengai Ole Sabaya, Mkuu wa Wilaya ya Hai atakuwa na ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na Lwelwe Mpina, Mkuu wa Jeshi la Polisi Hai leo tarehe 29 Julai 2019, Jeshi hilo limesitisha mikutano hiyo hadi pale Ole Sabaya atakapomaliza ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

“Kutokana na ufinyu wa nguvu kazi. Hivyo kwa busara sisitisha ziara na mikutano unayotegemea kuifanya hadi Mhe. Mkuu wa Wilaya atakapomaliza ziara yake,” inaeleza barua hiyo.

Barua hiyo inaeleza kuwa, kama Mbowe na Sabaya wote wakifanya mikutano, kutatokea muingiliano wa mikutano na ziara, na kusababisha uvunjifu wa amani ambao utahatarisha usalama wa wananchi.

“Napenda kukutaarifu kuwa Mkuu wa Wilaya Mhe. Lengai Ole Sabaya ana ziara wilayani hapa tangu 24/7/2019 kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.

“Hivyo, kwasababu za kiusalama, kuingiliana kwa mikutano na ziara kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani ambao utahatarisha usalama wa wananchi,” inaeleza barua hiyo.,

Hata hivyo, Basil Lema ambaye ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, amesema mikutano ya hadhara ya Mbowe, imeahirishwa baada ya kufiwa na kaka yake, Alfred.

Alfred amefariki dunia jana tarehe 28 Julai 2019 ikiwa ni siku moja kabla ya Mbowe kuanza ziara ya mikutano ya hadhara kwenye jimbo lake la Hai mpaka tarehe 1 Agosti 2019.

error: Content is protected !!