JESHI la Polisi nchini Tanzania, limemtimua kazi ofisa wake kwa kukutwa na bangi, gongo, viroba pamoja na kujiunganishia umeme kinyume cha utaratibu. Anaandika Mwandishi Wetu, Arusha…(endelea).
Polisi huyo aliyetambulika kwa jina la F.1445 Koplo William, alifukuzwa baada ya Kenan Kihongosi, Mkuu wa Wilaya ya Arusha kuvamia nyumbani kwa askari huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi tarehe 7 Januari 2021, Salum Hamduni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha amesema, Kihongosi alivamia nyumbani kwa askari wake baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi.
Kamanda huyo amesema, mkuu huyo wa wilaya na timu yake walipofika nyumbani kwa Koplo William, miongoni mwa mambo waliyobaini ni pamoja na kujiunganishia umeme kinume cha sheria.

Pia, walikuta mafuta ya dizeli lita 85, gongo lita tano, misokoto ya bangi 20 na viroba vilivyokatazwa na serikali boksi 84 ambavyo vimekatazwa na serikali pia chupa zenye konyagi tisa.
Amesema, uvamizi huo ulifanywa tarehe 5 Januari 2021, saa tatu usiku katika Mtaa wa Muriet, Kata ya Sokoni One.
Kamanda Hamduni amesema, askari wengine watatu walikamatwa kwa tuhuma za rushwa baada ya kushawishi kutaka rushwa kutoka kwa Sammy Mollel, mmiliki wa Kampuni ya Gems and Rocks Venture.
Na kwamba, askari hao walimteka Lucas Mdeme, Meneja wa Kampuni ya kuuza madini ya Crown Lapidary, Arusha wakimtaka awape Sh. 30 milioni.
Askari waliohusika katika tukio hilo ni Gasper Paul (H.125) kutoka Kitengo cha Intelijensia Makao Makuu, Heavenlight Mushi (G.5134) kutoka Kitengo cha Intelijensia Mkoa wa Kinondoni na Bryton Murumbe (H.1021) aliyekuwa Polisi Kazi za Kawaida Dodoma.
Kamanda Hamduni amesema, upelelezi wa kesi zao umekamilika na sasa, majalada yao yanapelekwa kwenye ngazi nyingine kwa hatua zaidi.
Leave a comment