January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polepole: Serikali mbili hazitekelezeki

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Humphrey Polepole

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Humphrey Polepole akitoa ufafanuzi juu ya muundo wa Serikali katika Rasimu ya Katiba Mpya

Spread the love

MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humprey Polepole, ameapa kuwa muundo wa Muungano wa serikali mbili hautekelezeki.

Amesema, “Mpango wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuingiza ajenda ya serikali mbili ndani ya rasimu ya katiba, utaweza kuingiza nchi katika matatizo. Hii ni kwa sababu, serikali mbili ndani ya Muungano hazitekelezeki.”

Amesema kupenyeza muundo wa serikali mbili kwenye Bunge la Katiba, ni kiyume cha utaratibu na kuonya kuwa kwa vyovyote itakavyokuwa, “muundo wa serikali mbili ni mgumu na hauwezi kutekelezeka.”

Amesema, “Huwezi kwenda kuwaambia Wanzanzibar wafute vipengele kwenye katiba yao inayotambua Zanzibar ni nchi kamili na Rais wao sio mkuu wa nchi. Halafu wakakuelewa.”

Akizungumza kwa hisia kali kwenye kongamano lililoandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na Mtandao wa Wanawake na Katiba Mpya.

Alisema, katiba ya Jamhuri ya Muungano ina muundo wa serikali mbili. Kwa namna matatizo yalivyo, hakuna njia ya kutatua matatizo yaliyosababishwa na muundo huo.

“Zanzibar walitaka Muungano wa mkataba….maana yake ni kuvunja muungano. Lakini baada ya kujadiliana nao, wamesogea kwenye tatu na tunawasihi wengine wasogee hapa kwenye tatu tujadiliane…kitendo cha kubaki huko ni kutaka kuvunja Muungano,”amesisitiza.

Amesema, “Nchi mbili zinapoungana na kuwa na nchi moja; nchi mpya inayozaliwa huwa inapewa mamlaka na madaraka fulani. Nchi mbili zilizoungana zinabaki maeneo ya nchi iliyozaliwa, ambayo huwa yanawekewa utawala wa ndani na sio kuwa na dola huru.

Mkataba huo ulitamka kwamba “ Zanzibar ibaki ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano, lakini itapewa vyombo vya kuratibu masuala ya watanzania waishio Zanzibar kwa ndani. Harafu Jamhuri ya Muungano itashughulika na mambo ya muungano na mambo ya Tanzania bara.”

“Zanzibar na Tanganyika ni maeneo ya Jamhuri . katiba ya Zanzibar ibara ya 1 inasema “ Zanzibar ni nchi” hivi unaweza kuwa na nchi ndani ya nchi nyingine,” amesisitiza.

Akizungumzia sababu zilizolifanya Bunge Maalum la Katiba kupoteza mwelekeo na pengine hadhi ya kusimamia mchakato wa katiba, Polepole amesema, kilichosababisha mpasuko katika Bunge la Katiba, ni kutofautiana kwa viongozi wakubwa waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Viongozi hao wakubwa ndani ya serikali wametofautiana kuhusu muundo wa Muungano.

“Makatibu wakuu wa Zanzibar wanataka serikali tatu lakini mambo ya Muungano yapungue na makatibu wakuu wa Tanzania Bara, wanataka serikali mbili lakini mambo ya muungano yaongezeke. Hapa kuna tatizo.”

Aidha, ametaja sababu nyingine ni kuvunjwa kwa mkataba wa Muungano mwaka 1964.

Kuhusu kupitisha katiba mpya iliyopendekezwa bila ya Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA) kushiriki amesema, “Hatuwezi kupata katiba inayopendekezwa kama wajumbe wa UKAWA hawatarudi bungeni.

Amesema, “Katiba inayopendekezwa ni lazima iungwe mkono kwa wingi wa theruthi mbili ya wajumbe wote toka bara na Zanzibar. kwa wale waliotoka nje ya bunge kwa upande wa Zanzibar idadi haiwezi kutimia. Hivyo hawawezi kuipitisha.”

Polepole amesema, sheria inasema lazima wakubaliane na sio kulazimishana. Wakibadili vifungu na kuipitisha bila UKAWA haitakuwa katiba ya wananchi bali katiba ya kununua watu.

error: Content is protected !!