August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Polepole: Bado naamini serikali tatu

Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM (kulia), akiteta jambo na Jaji Joseph Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Katiba

Spread the love

SIKU tatu tangu Humphrey Polepole ateuliwe kuwa katibu mpya wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapindizi (CCM), amesema hajabadilisha msimamo wa kuamini katika Muungano wa mfumo wa serikali tatu, anaandika Charles William.

“Mimi ni mwanachama wa CCM kwa imani. Msimamo wangu kwa taifa langu ni madhubuti. Ninaamini katika msingi wa kusema ukweli daima na fitina kwangu ni mwiko, iliyo kweli nitaisema kweli kama ilivyo na huwa sibadilishi maneno,” amesema.

Polepole ametoa kauli hiyo wakati wa makabidhiano ya ofisi aliyokuwa akiishikilia Nape Nnauye kwenye ofisi ndogo za Makao Makuu ya CCM Lumumba, Dar es Salaam. Uteuzi wa Polepole ambaye sasa atalazimika kuacha kuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, aliteuliwa katika vikao vya ngazi ya juu vya CCM vilivyofanyika Ikulu mwishoni mwa wiki.

Kwa kujulikana msimamo wake wa kutaka katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iwe inayotambua mfumo wa muungano wa serikali tatu, Polepole aliulizwa swali kama bado anabaki na msimamo huo hata baada ya kuteuliwa.

Swali limetokana na ukweli kwamba sera ya CCM kuhusu mfumo wa serikali, siku zote imekuwa ya kuamini mfumo wa serikali mbili na ndiwo umetajwa katika katiba inayopendekezwa ambayo ilipitishwa kwa nguvu kubwa ya ushawishi wa chama hicho baada ya kambi ya upinzani kutoka kwa kuona CCM inashinikiza katiba inayokidhi matakwa yake ya kisiasa.

Wajumbe wa upinzani na baadhi ya waliotoka asasi za kiraia, walitoka nje ya mjadala wakati Bunge Maalum la Katiba lilipokuwa likijadili rasimu ya Katiba mpya iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Polepole alikuwa mmoja wa makamishna wa tume hiyo ambayo iliweka mfumo wa serikali tatu kuwa ndio unaofaa kwa sasa kama walivyoeleza wananchi walio wengi kupitia maoni yao wakati tume hiyo ikikusanya maoni.

Utaratibu wa kupatikana kwa katiba mpya ulisita baada ya bunge hilo kupitisha Katiba inayopendekezwa ambayo inahitaji kupelekwa kwa wananchi ili watoe kauli kama wanairidhia au laa. Serikali mpya haijaeleza hatua hiyo ya mwisho itatekelezwa lini.

Wakati wa kuunda serikali, Rais John Magufuli alimteua Polepole kuwa mkuu wa wilaya ya Ubungo, na utendaji wake umekuwa ukienda kimyakimya mpaka jina lake lilipotajwa mwanzoni mwa wiki kuwa atakuwa sasa mrithi wa Nape, ambaye atabaki kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Polepole ameeleza kuwa kuteuliwa kwake kushika nafasi hiyo mpya katika chama, ni uthibitisho kuwa CCM kinaweza kubadilika kulingana na wakati na kwamba kada yeyote anaweza kushika nafasi yoyote kulingana na uwezo wake.

“Naahidi kusimamia misingi ya CCM ikiwemo imani kwamba rushwa ni adui wa haki na ninaamini wana-CCM wakiifuata misingi yake kwa asilimia 60 tu basi Tanzania itapiga hatua kubwa katika maendeleo.

Amesema anatarajia kuona CCM ambayo watu wakimuona mtu mwenye nguo za kijani na njano wanajisikia amani; wamuite na kumueleza kero zao kwa kuamini atazifikisha kunakohusika,” amesema.

Kuhusu kukwama kwa mchakato wa Katiba mpya, Polepole amesema hadhani kama imekwama, kwani bado anaamini kupatikana Katiba mpya waliyoitaka wananchi kuna umuhimu wake, na kusisitiza, “mchakato unahitaji maridhiano baina ya pande zote, rais bado anaendelea kubadili utawala na ameahidi kuendeleza mchakato huo.”

“Kuna mabadiliko makubwa yanaendelea katika serikali na katika chama ili kufungua njia ya Tanzania mpya, kwa kuwa kukosoa na kukosolewa ni sehemu ya misingi ya CCM, ukifika wakati wa kuyajadili hayo tutajadili,” amesema.

Mbali na msimamo wa serikali tatu, Polepole ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuingia kwenye Tume ya Warioba, anaamini katika kuwepo Tume huru ya uchaguzi, kupunguza mamlaka ya Rais, kutenganisha mamlaka ya mihimili ya dola, kumwajibisha Mbunge, kuwa na serikali ndogo (idadi ya mawaziri isiyozidi 15), maadili na miiko ya uongozi, mgombea huru na ukomo wa vipindi vya kuwania ubunge.

error: Content is protected !!