CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimeeleza kutokuwa na simile kwa wanachama wake, waliopita kwenye kura za maoni kisha kukutwa na makandokando. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho amesema, kila mwanachama aliyeshiriki ‘uovu’ katika kura za maoni, atashikishwa adabu.
Polepole ametoa kauli hiyo leo Jumatano tarehe 5 Agosti 2020, wakati akizungumza na wanahabari kwenye ofisi ndogo ya chama hicho, Lumbumba jijini Dar es Salaam.
“Muwe watulivu sababu nyie Watanzania wanawaamini kwenye wigo wa uongozi, tulieni. Hatutawaangusha watu wanyenyekevu kwenye chama chetu, muwe na amani.
“Wale mliopiga mazonge tutawafundisha adabu kipindi hiki. Sababu ukifundishwa adabu ni vizuri tukupe ‘surprise’ ukapate kazi nyingine kwa sababu uongozi unaotweza Katiba yetu hauna nafasi,” amesema Polepole.
Vikao vya Kamati za Siasa za Mkoa za CCM kuwajadili wagombea hao vilivyoanza janana vinatarajiwa kukamilika leo Jumatano tarehe 5 Agosti 2020.
Vikao vya Kamati za Siasa za Mkoa za CCM vinafanyika baada ya mikutano mikuu ya CCM majimbo na wilaya kwa ajili ya kuchuja wagombea kufanyika.
Mikutano mikuu ya CCM ya majimbo kwa ajili ya hatua ya awali ya kupendekeza wagombea ilifanyika Julai 20 hadi 21, 2020 ikifuatiwa na vikao vya Kamati za Siasa za Wilaya vilivyofanyika tarehe 1 hadi 2 Agosti 2020.
Hata hivyo , vikao vya Baraza Kuu la Wazazi la CCM kupendekeza wabunge viti maalum kundi la wazazi vitafanyika tarehe 9 Agosti mwaka huu, huku Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) litafanya kura za maoni kwa wagombea wa ubunge viti maalum tarehe 10 Agosti 2020.
Baada ya vikao hivyo kufanyika, mapendekezo yake yatawasilishwa katika vikao vya NEC.
Kwa upande wa wagombea wa udiwani, tarehe 6 Agosti 2020 Vikao vya NEC ngazi ya mikoa vitafanya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa udiwani wakata na wadi pamoja na madiwani viti maalum.
CCM kilifungua zoezi la kutafuta wagombea wake katika uchaguzi huo tarehe 14 Julai mwaka huu, ambapo watia nia katika nafasi mbalimbali walianza kuchukua siku hiyo, na kisha kurejesha fomu hizo tarehe 17 Julai 2020.
Leave a comment