Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Pingamizi la Mbowe, wenzake katika kesi ya ugaidi lagonga mwamba
Habari za SiasaTangulizi

Pingamizi la Mbowe, wenzake katika kesi ya ugaidi lagonga mwamba

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano Dar es Salaam,  imetupilia mbali pingamizi la Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, la kupinga mahakama hiyo kusikiliza  mashtaka ya ugaidi yanayowakabili, kwa maelezo kwamba haina mamlaka hiyo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Pingamizi hilo limetupwa leo Jumatano, tarehe 1 Septemba, 2021 na mahakama hiyo, mbele ya Jaji Elinaza Luvanda.

Akitoa uamuzi wa shauri hilo, Jaji Luvanda amesema maombi ya washtakiwa hao katika pingamizi hilo hayana msingi, kwa kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza.

Baada ya pingamizi hilo kutupwa, mahakama hiyo inaendelea kusikiliza kesi hiyo.

Pingamizi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo jana tarehe 31 Agosti 2021 na mawakili wa Mbowe na wenzake, wakiongozwa na Peter Kibatala wakiiomba mahakama hiyo iwaache huru washtakiwa kwa madai kwamba haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka ya ugaidi yanayowakabili.

Lakini mawakili wa upande wa Jamhuri walipinga pingamizi hilo, wakidai kwamba hoja zake si sahihi kwa mujibu wa sheria.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, alidai kwamba tafsiri ya kwamba mahakama hiyo inasikiliza kesi za makosa ya rushwa na uhujumu uchumi peke yake, sio sahihi.

 

Akidai, mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza mashtaka hayo, baada ya makosa yaliyoko katika sheria ya kuzuia ugaidi, kuwekwa katika Sheria ya Uhujumu Uchumi, kufuatia mabadiliko ya sheria mbalimbali Na. 3 ya 2016.

Wakili Kidando aliiomba mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi hilo, kwa madai kwamba ina mamlaka ya kusikiliza mashtaka ya ugaidi, kwa sababu ni sehemu ya Mahakama Kuu ya Tanzania.

Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, alipinga maombi ya washtakiwa kulipwa fidia, akidai kwamba fidia hutolewa endapo mahakama itaona mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya washtakiwa husika, ni ya kutungwa.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi Na. 16/2021 yenye mashtaka ya ugaidi, imeanza kusikilizwa leo baada ya kuhamishiwa katika mahakama hiyo, ikitokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfani Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Lingwenya.

Mbowe na wenzake wanashtakiwa kwa mashtaka sita, ikiwemo la kula njama za kufanya ugaidi na shtaka la kutaka kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya,  yanayowakabili wote.

Shtaka la kufadhili vitendo vya ugaidi,  kwa kutoa fedha za kufadhili ugaidi, linalomkabili Mbowe peke yake.

Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya makosa hayo kati ya tarehe 1 hadi 5 Agosti 2021, katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na  Morogoro.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Hii hapa kauli ya Sheikh mpya mkoa wa Dar

Spread the loveSAA chache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi ya aliyekuwa Sheikh...

Habari MchanganyikoTangulizi

Breaking news! Mufti amng’oa Sheikh mkoa Dar

Spread the loveBARAZA la Ulamaa la Bakwata katika kikao kilichofanyika tarehe 1...

Habari za Siasa

Kamati ya Bunge yaitaka Serikali kuchunguza dawa za asili

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo...

Habari za Siasa

Kada NCCR-Mageuzi aliyepotea aokotwa porini akiwa taabani, hajitambua

Spread the love  MWENYEKITI wa Jumuiya ya Vijana ya Chama cha NCCR-Mageuzi,...

error: Content is protected !!