December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Pingamizi jingine la kina Mbowe latupwa

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, imekubali kupokea barua inayomthibitisha Askari Mpelelezi, Ricardo Msemwa, kuwa ndiye aliyepokea kitabu cha mahabusu, kutoka kwa msajili wa mahakama hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, tarehe 15 Novemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joakhim Tiganga, akitoa uamuzi madogo wa pingamizi la mawakili wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake.

Mawakili wa utetezi, walipinga kielelezo hicho Ijumaa iliyopita, wakidai, shahidi aliyeomba barua hiyo ipokelewe hana uwezo wa kufanya hivyo kisheria, kwa madai nyaraka hiyo ililengwa mahususi kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS), jijini Dodoma, na kuwa Msemwa siyo mtumishi wa ofisi hiyo hivyo barua hiyo haimhusu.

Pia, walidai shahidi huyo wa pili wa Jamhuri katika ushahidi wake, hakusema barua hiyo imemfikiaje na au kueleza uwepo wa jina lake katika nyaraka hiyo.

Jaji Tiganga amesema, mahakama hiyo imeipokea barua hiyo kwa kuwa ni nyaraka muhimu.

Jaji huyo amesema, mawakili wa utetezi watapima kuaminika kwa shahidi na au nyaraka hiyo wakati wa maswali ya dodoso.

“Kupokea nyaraka ni jambo moja lakini kupima uzito wa nyaraka ni jambo lingine. Katika kupima uzito wa nyaraka hiyo ni mahakama inaona kwamba ni wakati wa cross-examination,” amesema Jaji Tiganga

Amesema, “kwa maana hiyo mahakama inaona barua hiyo iliyokuwa inaenda ofisi ya taifa ya mashtaka na kwamba shahidi alipewa nakala. Basi Mahakama hii inaona ni nyaraka sahihi na kwa sababu hiyo mahakama inapokea barua.”

Jaji Tiganga amesema “upande wa utetezi wanayo nafasi wakati wa dodoso, wanaweza kumpima shahidi huyu kama mkweli au siyo mkweli. Kielelezo kinatakiwa kisomwe lakini ku- refer content- ili aweze kutambua nyaraka hiyo. Kwa hiyo basi kwa Kesi ya Robison Mwangisi siyo sahihi kutumika kwenye kesi hii.”

Jaji Tiganga amesema mahakama hiyo imelitupa mbali pingamizi kwa kuwa sheria ya ushahidi inaruhusu shahidi kuaminika kupitia ushahidi wake alioutoa kwa mdomo, na kwamba mahakama hiyo imethibitisha kuwa Msemwa ni shahidi wa kuaminika.

“Na kwa maoni yangu kama ambavyo upande wa utetezi siyo Chain of Custody (mlolongo wa utunzwaji kielelezo), siyo wa kawaida. Tunachopaswa kungalia kama alipata kielelezo kwa utaratibu. Ni kweli alipaswa kutoa -dispatch- lakini tayari shahidi ameshaonesha kwa mdomo namna gani ambavyo amepata ushahidi huo. Kwa Sheria ya ushahidi inasema kwamba shahidi anaeleza ushahidi wake kwa mdomo na ataweza kuaminika, labda iamuliwe vinginevyo,”

Awali, Mawakili wa utetezi waliweka pingamizi dhidi ya barua hiyo wakiiomba mahakama hiyo isiipokee ili kuthibitisha kuwa shahidi huyo Msemwa ndiye aliyepokea kitabu cha mahabusu, kutoka kwa msajili wa mahakama.

Baada ya Msemwa kuiomba mahakama hiyo ipokee barua kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri, katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Ling’wenya, yasipokelewe kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri, katika kesi ya msingi inayomkabili Mbowe na wenzake.

Kutupwa kwa pingamizi hilo, kunafikisha mapingamizi yaliyotupwa ya upande wa utetezi kufikia sita tangu kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa mwishoni mwa Agosti mwaka huu huku wakishinda mawali.

Wengine kwenye kesi hiyo mbali na Mbowe na Ling’wenya ni Adam Kasekwa na Halfan Bwire ambao wanatuhumiwa kwa kesi ya uhujumu uchumu yenye mashtaka ya kupanga njama za vitendo vya kigaidi.

Kesi hiyo inaendelea mahakamani. Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali.

error: Content is protected !!