January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Pinda azindua Wiki ya Elimu Dodoma

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwasikiliza wanafunzi katika ufunguzi wa Wiki ya Elimu, mjini Dodoma

Spread the love

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amezindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Elimu leo katika uwanja wa Jamhuri, mkoani Dodoma. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Maadhimisho hayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “Elimu bora ni haki ya kila mtoto kwa maendeleo ya Taifa”.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Pinda amesema chimbuko la maadhimisho ya Wiki ya Elimu yanatokana na mpango wa serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Result Now – BRN).

“Katika mpango huu, tulikubaliana sekta ya elimu, kuongeza motisha ya utoaji elimu, kwa kutoa tuzo kwa wanafunzi, walimu na shule zinazofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya taifa,” amesema Pinda.

Pinda amesema shughuli hiyo ilianza ngazi ya wilaya, mikoa na leo ni ngazi ya taifa huku maadhimisho yakijikita katika malengo makuu matatu.

“Kwanza ni kuwatambua wanafunzi, walimu, shule, Halmashauri na mikoa, ziliyofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba na ule wa kidato cha nne mwaka jana,” amesema Pinda.

Amesema lengo hilo litasaidia kuchochea ari ya ushindani wa kitaaluma na kuongeza ufanisi na uwajibikaji hususani katika kufundisha na kujifunza.

Lengo la pili, ni kuelimisha umma juu ya umuhimu wa elimu na nafasi aliyonayo kila mwananchi katika kuchangia maendeleo ya elimu kwa watoto.

“Lengo la tatu ni kupata nafasi ya kutathimini matokeo yetu na changamoto zilizopo katika elimu na jinsi ya kukabiliana nazo kwa pamoja. Aidha, ni nafasi ya sisi kama serikali kupata mrejesho na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali juu ya uimarishaji wa elimu nchini ili kuleta maendeleo kwa taifa,” ameongeza Pinda.

Kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Ijumaa wiki hii, huku Rais Jakaya Kikwete akitarajiwa kuwa mgeni rasmi ambapo atatoa tuzo kwa wanafunzi, walimu na shule zenye ufaulu uliotukuka.

error: Content is protected !!