July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Pinda atamani “akina Nyambui” wengine

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akifungua michezo ya Umiseta na Umitashumta jijini Mwanza

Spread the love

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amewahimiza wachezaji wanaoshiriki michezo ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari (Umisseta) na Msingi (Umitashumta) kufuata nyayo za wachezaji waliong’ara ndani na nje ya nchi kama Selemani Nyambui. Anaandika Moses Mseti … (endelea).

Pinda alitoa kali hiyo jana wakati wa uzinduzi wa michezo hiyo inayoendelea jijini Mwanza, akisema kufuata nyayo za wanariadha waliong’ara miaka ya nyuma kama Suleiman Nyambui, Filbert Bayi, Juma Ikangaa na Mwinga Mwanjara, kutasaidia kuing’arisha nchi kimataifa.

Amesema lazima washiriki wa michezo hiyo waelewe umuhimu wa michezo huku serikali ikiendelea na dhamira ya kuwaandaa vijana wawe wana michezo mahiri na washindani kimataifa.

Kwa mujibu wa Pinda, michezo hiyo ni fursa nzuri kwa vijana kuimarisha vipaji vyao pamoja na kulitambulisha taifa kimataifa zaidi.

“Michezo inakomaza akili, nidhamu na kuibua vipaji maalum…hii michezo ni maandalizi mazuri kwa wachezaji kushiriki michezo ya shirikisho ya shule za sekondari za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baadaye,” amesema.

Hata hivyo, Pinda amesema michezo nchini ina changamoto mbalimbali zikiwamo za kutokuwa na wataalam wa kutosha, wanafunzi kutofundishwa somo la michezo kuanzia ngazi za msingi hadi vyuoni pamoja na viwanja kutotunzwa.

Waziri Mkuu aliziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha viwanja vilivyopo sehemu ya wazi kutovamiwa na kuvilinda kwa ajili ya michezo kwa watoto.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, amesema michezo hiyo mwaka huu inajumuisha washiriki 1,755 kwa upande wa Umisseta na Umitashumta washiriki ni 1,000.

Ghasia amesema mashindano ya Umisseta yalianza Juni 8 na kuhitimishwa Juni 20 mwaka huu, wakati yale ya Umitashumta yataanza Juni 22 na kumalizika Julai 4 mwaka huu, katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Butimba, jijini Mwanza.

“Mashindano haya yanasaidia kuibua na kujenga vipaji imara kwa vijana pamoja na kujielimisha kitaaluma zaidi pamoja na dhana ya kujiamini,” amesema Ghasia.

Amesema michezo hiyo inashirikisha kanda 11 zikiwamo mbili za Zanzibar na Pemba pamoja na zote za Tanzania Bara.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, Zuberi Tawasaba, amesema mashindano hayo yanashirikisha wanafunzi wa sekondari wa kuanzia kidato cha kwanza hadi sita, walioanzia kushindana ngazi za shule, kata, wilaya, mkoa na sasa taifa.

“Tangua yaanzishwe 1969, haya ni mashindano ya 37, lakini ni ya nane tangu yazinduliwe upya na Rais Jakaya Kikwete 2007 baada ya kusitishwa mwaka 2000 kutokana na kuwapo na changamoto mbalimbali zikiwamo za kuchangishwa wazazi fedha,” amesema Tawasaba.

error: Content is protected !!