WATU 10 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kujihusisha na wizi wa pikipiki. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Akizungumza na wanahabari leo Jumatatu tarehe 1 Machi 2021 jijini Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema, watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni maalumu ya kusaka wezi wa pikipiki.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kuanzia tarehe 1 hadi 28 Februari 2021, lilifanya oparesheni maalum ya kuwasaka wezi wa pikipiki na kufanikiwa kuwakamata wakiwa na pikipiki 16 zidhaniwazo kuwa za wizi,” amesema Kamanda Mambosasa.
Miongoni mwa watuhumiwa hao ni, Stephen Paul (38), Mkazi wa Ulongoni A, Salum Mustafa (28), Mkazi wa Kigogo na Nsajigwa Kaisi (25), Mkazi wa Mongo la Ndege A.
“Oparesheni hiyo ilifanyika baada ya kupokea taarifa toka kwa wahanga wa matukio hayo ambayo yalikithiri katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam.
“Aidha watuhumiwa hao wamekuwa wakiiba pikipiki katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kuzipeleka kwa madalali ili kuziuza sehemu mbalimbali,” amesema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa amesema, Jeshi la Polisi, Kanda Maalum Dar es Salaam linaendelea na oparesheni ya msako wa wizi wa pikipiki, magari na wahalifu wa makosa mengine.
Leave a comment