September 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Pigo lingine kwa Maalim Seif, mahakama yamtambua Prof. Lipumba  

Spread the love

HATIMAYE Mahakama Kuu, Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo tarehe 18 Machi 2019 imetoa uamuzi kwamba, Prof. Ibrahim Haruna Lipumba ni mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi (CUF). Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akitoa ufafanuzi wakati wa kusoma uamuzi wa mahakama hiyo kuhusu uenyekiti wa Prof. Lipumba, Jaji Benhajj Masoud wa mahakama hiyo amesema, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haaishi kusajili tu, inaweza hata kufuta chama.

“Nimeridhika na hiki ambacho kimetolewa ndani ya kiapo cha mjibu maombi namba moja (msajili wa vyama saisa) kwamba, kama hana mamlaka ya kukifuta chama basi hana mamlaka ya kumrejesha Profesa Lipumba kwenye kiti chake,” Jaji Masoud na kuongeza;

“Msajili wa vyama vya siasa haishii kusajili chama tu, ndio maana sheria imempa mamlaka ya kufuta chama hivyo basi anamamlaka hayo,” ameeleza Jaji Benhajj Masoud wakati akitoa uamuzi wa uhalili wa Prof. Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF.

Awali uamuzi wa kesi hiyo ulitarajiwa kutolewa tarehe 22 Februari 2019, iliahirishwa kwa amelezo kwamba, jaji amepangiwa majukumu mengine nje ya mahakama.

Kwenye kesi hiyo Prof. Lipumba alishitakiwa kuwa si mwenyekiti halali wa CUF kwa kuwa, alijiuzulu kwa hiari yake kupitia tamko lake kwa waandishi wa habari hapo tarehe 5 Agosti 2015.

Kwenye andishi lake hilo Prof. Lipumba alisema, hawezi kushika wadhifa huo kutokana na kukosa ushirikiano wa viongozi wenzake.

Alisema namna chama kinavyokwenda, nafsi yake inamsuta kuendelea kuwa kiongozi wake; ila anakusudia kubakia mwanachama muaminifu na iwapo chama kitaridhia awe tu mshauri wake.

Prof. Lipumba alishikilia uamuzi wake wa kujiuzulu licha ya kunasihiwa na viongozi wenzake wa juu akiwemo Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad.

Hukumu hiyo imekuja ikiwa ni siku nne baada ya Prof. Lipumba kuchaguliwa kwa mara nyingine kuwa mwenyekiti wa chama hicho huku Maalim Seif akiwekwa nje ya chama hicho baada ya kambi ya Lipumba kumchagua Halifa Suleiman Halifa kushika wadhiba huo.

Habari zaidi zitakujia…

error: Content is protected !!